Na. Mussa Richard, DODOMA
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, ametoa wito kwa wananchi jijini Dodoma kutumia nishati safi ya kupikia ili kutunza mazingira na kulinda afya za wananchi kutokana na madhara ya matumizi ya nishati chafu ya kupikia.
Senyamule alisema hayo wakati wa mkutano wa hadhara katika Kata ya Nzuguni, baada ya kufanya ziara na kukagua miradi mbalimbali ya maendelea katika kata hiyo.
“Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania ameshaelekeza kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia nyumbani na katika sehemu za mikusanyiko, kwahiyo kama huwezi kununua mtungi wa gesi ni bora zaidi ukatumia nishati mbadala kama makaa ya mawe na kuni poa, kwasababu upatikanaji wake na gharama zake ni nafuu na rafiki kwa kila mmoja wetu kuweza kuzimudu, hilo litasaidia kuondokana na madhara ya kiafya yatokanayo na matumizi ya nishati chafu za kupikia, lakini pia itasaidia kutunza mazingira ya jiji letu na kuondokana na uhalibifu kama ukataji wa mkaa” alisema Senyamule.
Nae Jabir Shekimweri, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma akazitaka taasisi zote kwa pamoja kutumia ipasavyo nishati safi ya kupikia ili kuondoa madhara ya uharibifu wa mazingira katika Jiji la Dodoma na kuwa mfano kwa taasisi za mikoa mingine kuiga na hatimaye kuwa na Tanzania inayotunza mazingira kwa vitendo.
“Katika masuala ambayo serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania chini ya Rais, Samia Suluhu Hassan imevipa kipaumbele ni sekta ya nishati safi ya kupikia, kwasababu serikali imeona uharibifu na madhara makubwa ambayo yanasababishwa na matumizi ya nishati chafu ya kupikia, na mwisho wa kampeni hii ya kuhakikisha wananchi kote nchini wanatumia nishati safi ya kupikia ilikua mwisho mwezi Desemba mwaka jana, na nikatoa tamko kuwa hatutarajii tena kukuta sehemu yenye mkusanyiko wa watu zaidi ya 100 bado wanatumia nishati chafu ya kupikia kama, mkaa na kuni” alisema Shekimweri.
Ziara hiyo ilihitimishwa kwa mkutano wa hadhara kati ya Mkuu wa mkoa na wanachi wa Kata ya Nzuguni, uliofanyika uwanja wa ofisi ya Kata ya Nzuguni ambapo alisikiliza na kutatua kero mbalimbali za wananchi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.