Angela Msimbira, OR-TAMISEMI
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Dkt.Festo Dugange amesema serikali kwa kushirikiana na wadau wa elimu nchini inaendelea kuchukua hatua stahiki kuhakikisha vitendo vya unyanyasaji na ukatili dhidi ya watoto ikiwemo mimba na ndoa za utotoni zinatokomezwa nchini.
Ameyasema hayo leo tarehe 9 Septemba, 2022 jijini Dodoma kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwenye hafla fupi ya utoaji wa zawadi kwa wanafunzi waliofanya vizuri kwenye insha iliyohusu mimba na ndoa za utotoni.
Amesema kuwa Serikali imeendeleza jitihada za kudhibiti ndoa na mimba za utotoni ambapo kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ambayo imekuwa ikitoa sera, Waraka na miongozo mbalimbali ili kukabiliana na changamoto hizo ambapo Ofisi ya Rais-TAMISEMI imeendelea kusimamia utekelezaji wake.
Dkt. Dugange ametaja miongozo na Waraka zilizotolewa ili kukabiliana na mimba na ndoa za utotoni kuwa ni Waraka wa Elimu Namba mbili wa mwaka 2008 na kuanzishwa kwa mwongozo wa Mwaka 2022 wa kurejesha shuleni wanafunzi waliokatiza masomo katika elimu ya msingi na sekondari.
Ameendelea kufafanua kuwa katika mwaka 2016 hadi 2022 Serikali imefanya mageuzi makubwa katika sekta ya elimu hususani katika bajeti ya elimu bila ada na ujenzi wa miundombinu ya shule lengo likiwa ni kuboresha elimu msingi na sekondari.
Aidha, amesema kuwa kuwalinda wanafunzi wasiingie kwenye changamoto mbalimbali serikali imeweza kuboresha miundombinu ya shule za msingi na sekondari kwa kujenga madarasa na mabweni.
Dkt. Dugange ametoa rai kwa viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kufanya jitihada za kuwatambua wadau wa elimu waliopo katika maeneo yao kuhakikisha wanawashirikisha katika kutatua changamoto zilizopo badala ya kusubiri kila changamoto itatuliwe na Serikali.
Naye, Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi ya World Vision Tanzania, Dkt.Diana Mdeme ameiomba Serikali kuendelea kusimamia sheria na kuchukua hatua stahiki kwa wanaohusika katika kusababisha mimba na ndoa za utotoni.
Chanzo: Tamisemi
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.