Na. Dennis Gondwe,
Serikali imeamua kutoa chanjo ya ugonjwa wa virusi vya Korona (UVIKO-19) kwa wananchi wake kwa lengo la kupunguza madhara na vifo vitokanavyo na ugonjwa huo nchini ili wananchi hao waweze kushiriki katika shughuli za kujiletea maendeleo.
Kauli hiyo ilitolewa na Afisa Muuguzi Mwandamizi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Lorner Mziray (pichani) alipokuwa akiongea na wananchi wa Mtaa wa Nzasa katika Kata ya Chihanga jijini hapa leo.
Mziray alisema kuwa serikali imeruhusu chanjo ya UVIKO-19 itumike nchini kwa lengo la kuwahakikishia uhai wananchi wake dhidi ya ugonjwa huo. “Baada ya serikali kujiridhisha na usalama wa chanjo ya UVIKO-19, ikaruhusu chanjo hiyo itumike nchini ili kupunguza vifo vilivyokuwa vikitokea kutokana na ugonjwa huo. Hivyo, chanjo hii ni muhimu na salama kwa wananchi. Chanjo hii itatusaidia kuwa salama na kuendelea kutekeleza majukumu yetu ya kujiletea maendeleo kwa sababu inapunguza madhara makubwa yatokanayo na UVIKO-19, na vifo” alisema Mziray.
Akiongelea madhara ya UVIKO-19, aliyataja kuwa ni mapafu kupoteza uwezo wa kufanya kazi kama kawaida. Madhara mengine ni vifo, jambo linalopunguza nguvu kazi ya familia na taifa kwa ujumla. “Watoto kupoteza wazazi wao na kuishia kuwa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi na kupoteza ndoto zao za elimu na maisha bora” alisema Afisa Muuguzi Mwandamizi huyo.
Alisema kuwa chanjo hiyo ni muhimu sana kipindi hiki ambapo ugonjwa huo hauna tiba. “Serikali inapenda wananchi wote wenye umri wa kuanzia miaka 18 waweze kupata chanjo ya UVIKO -19. Chanjo hiyo ni silaha kwa kuwapunguzia wananchi madhara makubwa yatokanayo na ugonjwa huo. Msisitizo mkubwa kwa serikali ni makundi maalum ya wazee, watu wenye magonjwa sugu kama kisukari, shinikizo la damu, figo, na virusi vya Ukimwi kuchanja. Bahati nzuri chanjo hii inatolewa bila malipo na kwa hiari” alisema Mziray.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.