WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt.Pindi Chana amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi wenye nia ya kutaka kuwekeza kwenye sekta ya utalii nchini ili kuweza kutafsiri kwa vitendo maono ya Rais Samia kupitia filamu ya The Royal Tour
Alitoa kauli hiyo jijini Dar-es-salaam wakati akizungumza na Chama cha Mawakala wa usafiri wa anga Tanzania (TASOTA) kwenye mkutano wao wa mwaka ambapo kila mwaka hukutana mara moja kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali kuhusu ustawi wa Chama chao.
Alisema Serikali imepunguza ada ya kila mwaka kwa Mawakala wa Usafiri wa anga nchini (TALA fee) kutoka dola za Marekani 2,000 hadi dola 500
Pia alieleza kuwa Serikali imejipanga kupunguza utitiri wa kodi katika sekta ya utalii ili kuhamasisha wawekezaji zaidi katika sekta hiyo hivyo, kupelekea kutoa ajira nyingi zaidi.
Aliongeza kuwa Serikali imeendelea kuwekeza miundombinu bora katika maeneo ya Hifadhi ikiwemo barabara zenye uwezo wa kupitika muda wote pamoja na usimikaji wa mtandao wa intaneti katika mlima Kilimanjaro.
Amesisitiza kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi ili kuondoa vikwazo kwa wadau wenye nia ya kutaka kuwekeza hapa nchini.
Akizungumzia umahiri wa TASOTA, Waziri Chana alisema wanachama hao wamekuwa wazalendo na Mabalozi wa kutangaza vivutio vya utalii nchini kwa wageni wanaotaka kuja kujionea uzuri wa Tanzania
”Najisikia fahari kuona TASOTA, wakifanya kazi usiku na mchana ya kuilinda na kuitetea taswira ya nchi kwa kuratibu na kupanga safari za watalii wanaotembelea Tanzania ”
Aidha, Dkt.Chana ameihaikikishia TASOTA kuwa yeye kama Waziri mwenye dhamana ataendelea kufanya kazi kwa ukaribu na jumuiya hiyo ili sekta ya utalii iweze kuleta matokeo yaliyokusudiwa.
Naye Mwenyekiti wa TASOTA, Moustafa Khataw amesema anaishukuru Serikali kwa kutambua mchango wao wa kutangaza uzuri wa Tanzania
”Tumekuwa tukifanya kazi zetu kwa weledi wa hali ya juu katika tasnia ya usafirishaji kwani biashara hii haina njia za mkato wala haina ujanja ujanja inahitaji watu wazalendo na wenye haiba nzuri katika kuwahudumia watalii wetu, ” alisema Mwenyekiti Khataw.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.