OFISI ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa imesema itaendelea kutoa ushirikiano kwa mamlaka za Serikali za mitaa ili ziweze kutekeleza majukumu yake ya kuwaletea maendeleo Wananchi.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo katika hotuba yake wakati wa hafla ya utiaji saini mkataba wa ushauri katika utafiti na usanifu wa mfumo wa utiririshaji wa maji ya mvua na maandalizi ya mpango wa uboreshaji wa mifumo ya mitaro ya maji ya mvua na maji taka katika jiji la Dodoma kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2020 hadi 2040.
“Ofisi ya Rais TAMISEMI itaendelea kutoa ushirikiano kwa mamlaka za Serikali za Mitaa ili ziweze kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria” alisema Jafo.
Akiongelea utekelezaji wa mkataba huo, alisema kuwa mshauri msanifu ni mtu muhimu sana katika ufanisi wa mradi na kuwa, anategemea kazi ya utafiti na usanifu katika mradi huo itafanyika vizuri ili kuondoa matatizo yanayozuilika wakati wa utekelezaji wa mradi huo.
“Tunataka wakati wa utekelezaji wa mradi huu ujibu shida za wananchi katika jiji la Dodoma, tunataka Jiji hili lipangwe vizuri na watu waje kutoka maeneo mengine kufanya utalii Dodoma” alisisitiza.
Aidha, Waziri Jafo alitoa pongezi kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kusimamia shughuli za Halmashauri hiyo kwa weledi mkubwa.
“Pongezi kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kufanya kazi nzuri, naomba Mungu asaidie ubaki hapa ili uendeleze mazuri yako” alisema.
Wakati huo huo, Waziri Jafo ameipongeza Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kufanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato. “Jiji la Dodoma ndiyo Jiji pekee linaloongoza kwa ukusanyaji wa pato ghafi kwa Halmashauri zote nchin...hongereni sana Jiji la Dodoma kwani mapato yenu ya ndani yanaweza kuendesha Halmashauri nyingine bila serikali kuu kuongeza fedha, Hakika Dodoma ni Jiji la mfano hongereni sana” alisema Waziri Jafo.
Awali, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi alisema kuwa mradi wa ushauri katika utafiti na usanifu wa mfumo wa utiririshaji wa maji ya mvua na maandalizi ya mpango wa uboreshaji wa mifumo ya mitaro ya maji ya mvua na maji taka katika Jiji la Dodoma kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2020 hadi 2040 unalenga kukidhi mahitaji halisi ya Jiji pamoja na kutunza mandhari.
Kunambi alisema kuwa, usanifu wa mradi huo utatoa suluhisho la kudumu katika kupambana na mafuriko ya mara kwa mara katika Jiji la Dodoma ambapo utaweka mfumo thabiti wa ukusanyaji wa maji taka ili kuhakikisha mazingira ya jiji yanabaki kuwa nadhifu wakati wote.
Mradi huo utatekelezwa na mshauri msanifu kampuni ya Cheil Engineering Co. Ltd kutoka Jamhuri ya Korea Kusini kwa kushirikiana na kampuni ya AJOMA Consult Ltd. ya Tanzania kwa mkataba wenye gharama ya Shilingi 1,575,573,813.10, ambao utatekelezwa kwa muda wa miezi 12 kuanzia tarehe Mei 6, 2019 mpaka Mei 5, 2020.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.