SERIKALI ya awamu ya sita imejizatiti kulifanya Jiji la Dodoma kuwa la kisasa kwa kuboresha miundombtinu na huduma za tiba za kibingwa na kuwahakikishia wananchi maisha bora.
Kauli hiyo ilitolewa na Rais wa awamu ya sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alipokuwa akiwahutubia mamia ya wananchi wa Dodoma na mikoa ya jirani waliojitokeza katika hafla ya uzinduzi wa mkakati wa uelimishaji na uhamasishaji wa Sensa ya watu na makazi katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma leo.
“Waheshimiwa viongozi na ndugu wananchi, kwa kuwa nipo hapa Dodoma siwezi kuhitimisha hotuba yangu bila kusema machache kuhusiana na mipango ya serikali kwenye jiji hili. Kwanza kabisa nataka niwathibitishie kuwa adhima na dhamira ya serikali kuifanya Dodoma kuwa jiji la kisasa ipo palepale” alisema Rais Samia.
Akiongelea uboreshaji wa huduma, alisema kuwa serikali inaendelea na kuboresha miundombinu ya huduma. “Tunaendelea na ujenzi wa miundombinu ya kuboresha matibabu ya kibingwa kwenye hospitali ya rufaa ya Mkoa na hospitali ya rufaa ya Benjamini Mkapa” alisema Rais Samia.
Kwa upande wake mwenyekiti wa kamati ya taifa ya sensa, Kassim Majaliwa alisema kuwa serikali imelenga kujenga uchumi wa viwanda. “Mheshimiwa Rais serikali yako ya awamu ya sita imelenga kuwahudumia ipasavyo wananchi na kujenga uchumi wa viwanda. Pia ufuatiliaji wake umebainishwa katika Mpango wa III wa maendeleo wa mwaka 2021/2022 hadi mwaka 2025/2026 kwa lengo la kupanua wigo wa uchumi kwa mtu mmoja mmoja lakini pia na Taifa pamoja na kuongeza ajira kwa vijana wetu na hatimae kupunguza umasikini. Haya yote Mheshimiwa Rais hayawezi kutekelezwa bila ya kuwa na takwimu zenye ubora stahiki” alisema Majaliwa.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.