RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli jana tarehe 05 Novemba 2020 ameapishwa kuanza muhula wa pili wa uongozi wa awamu ya tano katika sherehe iliyofanyika uwanja wa Jamhuri hapa Jijini.
Akizungumza na Wananchi pamoja na wageni mbalimbali mara baada ya kuapishwa Dkt. Magufuli pamoja na mambo mengine alishukuru na kuipongeza kamati ya maandalizi.
"...naishukuru na kuipongeza Kamati ya maandalizi kwa matayarisho mazuri kwa hakika sherehe imefana sana, kwa sababu watu wamejaa ndani ya uwanja lakini wamejaa pia nje ya uwanja, hii inanipa changamoto Serikali itakayoanza leo (jana), kwamba kitu cha kwanza tutaanza kujenga uwanja mkubwa sana hapa Dodoma. Ili sherehe zingine zitakapokuja watu wote wa Dodoma waweze kuwa ndani ya uwanja na washerehekee vizuri.
Navishukuru sana vyombo vya habari, kwa kufanya kazi kwa weredi na uzalendo mkubwa tangu kuanza kwa kampeni mpaka leo tunapokamilisha shughuli za uchaguzi, asanteni na hongereni sana wana habari kwa kazi kubwa mliyofanya" alisema Dkt. Magufuli.
Nao baadhi ya wananchi waliohojiwa na tovuti hii kuhusiana na kauli ya Rais Dkt. Magufuli kuhusu ujenzi wa uwanja, wengi wameipokea kwa furaha na matumaini makubwa hasa baada ya kuona utekelezaji wa miradi na miundombinu mbalimbali katika muhula wa kwanza wa Serikali ya awamu ya tano.
"Tangu Dodoma imepandishwa hadhi kuwa Jiji imekua na kuongezeka sana katika awamu hii ya tano, ongezeko la watu lililotokana na ujio wa Serikali kuhamia Dodoma, kuongezeka kwa shughuli za kitaifa na kimataifa na hata Jiji la Dodoma kuwa na timu mbili zinazoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara yaani timu za Dodoma Jiji FC inayomilikiwa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma na timu ya JKT Tanzania, imesababisha kuwe na uhitaji wa uwanja mkubwa, na kwa kweli tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kuliona hilo". Alisema John Lugendo mkazi wa eneo la Nkuhungu hapa jijini.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.