SERIKALI kupitia Wizara ya Kilimo inakamilisha taratibu za ujenzi wa Vituo vitatu vya ukusanyaji, uhifadhi na utengaji wa madaraja kwa lengo la kuwezesha ufanisi na ubora katika usafirishaji wa mazao ya mboga mboga na matunda kutoka mashambani mpaka kumfikia mlaji wa mwisho ndani na nje ya nchi. Vituo hivyo vitajengwa katika bandari ya Dar es Salaam, Siha mkoani Kilimanjaro na Mufindi Mkoani Iringa.
Hayo yamesemwa leo tarehe 28 Novemba, 2022 na Naibu Waziri wa Kilimo, Mh. Anthony Mavunde alipokuwa akifungua Kongamano la Kimataifa la uthibiti ubora na viwango vya mazao ya mbogamboga na matunda lililofanyika Jijini Arusha.
"Hatuwezi kufikia ubora wa masoko ya kimataifa ya mazao yetu ya mboga mboga na matunda nchini pasipo kujenga miundombinu wezeshi.
Serikali kupitia Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, imetoa fedha kwa ajili ya kuwezesha ujenzi wa Vituo vitatu vya ukusanyaji na uhifadhi wa mazao (common use facility) hayo ili yaweze kusafirishwa kwa ubora na viwango vya kimataifa.
Lengo ni kutoa kipaumbele kwa mazao ya mboga mboga na matunda kuanzia yanaposafirishwa kutoka mashambani mikoani mpaka yanaposafirishwa bandarini, mipakani ama kwenye viwanja vyetu vya ndege. Ni dhahiri kwamba mazao ya mboga mboga na matunda hayawezi kusafirishwa kwa kipaumbele sawa na bidhaa kama madini ya shaba au makaa ya mawe, lazima tuyape kipaumbele ili kutoharibu ubora wake.
Serikali imepanga kuongeza mapato kutokana na mauzo ya bidhaa za matunda na mboga mboga nje ya nchi kutoka Dola za Kimarekani milioni 750 hadi bilioni 2 ifikapo Mwaka 2030. Ni matarajio yetu kwamba kama Nchi, tunashirikiana kwa pamoja Serikali nanyi wadau wote, kuweka mifumo thabiti ya ubora wa mazao yetu tunayouza nje ya nchi” Alisema Mavunde.
Awali, Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi Kilele ya Wadau wa Mazao ya Horticulture (TAHA), Dkt. Jacqueline Mkindi alieleza lengo la kongamano hilo ni kutathmini mbinu bora za kilimo, kuangalia nafasi ya Nchi yetu ya Tanzania katika ushindani wa masoko ya Kimataifa, kuongeza wigo wa upatikanaji wa masoko ya uhakika na kuendelea kuelimishana juu ya uthibiti wa viwango vya ubora wa mazao yetu yanayouzwa nje ili kuongeza pato la mkulima na Taifa kwa ujumla.
Wakati huohuo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Taasisi ya TAHA, Mhandisi Zebadiah Moshi alishukuru ushirikiano wa dhati wa Serikali na kuongeza kuwa, baada ya mkutano huo wakulima wanaenda kuongeza uelewa wa namna ya kufikia viwango vya kimataifa na hivyo kuongeza mauzo ya nje.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mheshimiwa John Mongella alishukuru kwa mkutano huo kufanyika Mkoani Arusha, na kusisitiza kuwa milango ya Serikali ya Mkoa wa Arusha ipo wazi kwa TAHA na wadau wote kwenye mnyororo wa thamani wa mazao ya mboga mboga na matunda hivyo wakaribie watapata ushirikiano mkubwa katika jitihada za kuinua maisha ya wananchi na pato la Taifa kwa ujumla.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.