RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewathibitishia wakazi wa Dodoma kuwa dhamira ya serikali kulifanya Jiji la Dodoma kuwa la kisasa ipo palepale kwa kuboresha miundombinu na huduma za kijamii.
Rais Samia alitoa hakikisho hilo kwa wakazi wa Dodoma alipokuwa akiwahutumia maelfu yao waliojitekeza katika hafla ya uzinduzi wa mkakati wa uelimishaji na uhamasishaji wa Sensa ya watu na makazi mwaka 2022 katika uwanja wa Jamhuri jijini hapa.
Rais Samia alisema “waheshimiwa viongozi na ndugu wananchi, kwa kuwa nipo hapa Dodoma, siwezi kuhitimisha hotuba yangu bila kusema machache kuhusiana na mipango ya serikali kwenye jiji hili. Kwanza kabisa nataka niwathibitishie kuwa adhima na dhamira ya serikali kuifanya Dodoma kuwa Jiji la kisasa ipo palepale. Hivi majuzi mlishuhudia Waziri Mkuu alikwenda kukagua ujenzi wa Ikulu mpya ambapo umefikia asilimia 75”.
Akiongelea ujenzi wa miundombinu ya barabara, alisema inaendelea vizuri. “Kuhusu ujenzi wa miundombinu, kama mnavyofahamu tayari tumesaini ujenzi wa barabara ya mzunguko ya njia nne. Ujenzi umechelewa kuanza kidogo kwa sababu ya matatizo ya fidia. Hata hivyo, changamoto hiyo tunakaribia kuimaliza na muda si mrefu ujenzi wa barabara hiyo utaanza” alisema Rais Samia kwa uhakika.
Rais aliipongeza kamati ya maandalizi kwa kukamilisha mkakati wa uelimishaji na uhamasishaji wa Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 mapema. “Nimeupitia mkakati huu, nami nimeridhika nao. Niwashukuru wale wote waliosaidia kwenye mkakati huu. lakini watakaosaidia mpaka tutakapofikia kufanya Sensa mwaka 2022. Jukumu letu ni kwenda kuutekeleza mkakati huu” alisema Rais Samia akionesha matumaini makubwa.
Sensa ya watu na makazi mwaka 2022 inaongozwa na kaulimbiu isemayo “Sensa kwa maendeleo, Jiandae kuhesabiwa”.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.