SERIKALI kupitia Wizara ya Afya, Maendelo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo wanaochangia sekta ya afya kupitia Mfuko wa Afya wa Pamoja (Health Basket Fund) imeridhia kuweka saini Hati ya Shilingi Bilioni 125.69 kwa ajili ya kuimarisha huduma za afya katika ngazi ya msingi nchini
Akiongea wakati wa kuidhinisha makubaliano hayo, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof. Mabula Mchembe amesema kuwa lengo kuu la Mfuko huo tangu kuanzishwa kwake mwaka 1999 ni Kuimarisha huduma za afya katika ngazi ya msingi (Halmashauri) zote nchini.
Amesema katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2020/21 Wadau nane (8) watachangia jumla ya USD 53.84 sawa na Shilingi bilioni 125.69 kwa kipaumbele cha kuimarisha huduma za afya katika vituo vya afya kwenye halmashauri zote 184 nchini.
“Shilingi bilioni 105.32 zitatumika kwa ajili ya kuimarisha utoaji wa huduma za afya katika vituo vya afya vipatavyo 5,533 kwenye halmashauri zote 184 nchini ikiwa ni pamoja na ununuzi wa dawa, vifaa na vifaa tiba, uendeshaji wa vituo, ukarabati mdogo na huduma za chanjo na vikoba. “Fedha hizo zitapelekwa moja kwa moja vituoni kwa utaratibu wa ‘Direct Health Facility financing” Alisema Prof. Mchembe.
Aidha, Prof' Mchembe alisema Shilingi bilioni 4.29 zitatumika kwa ajili ya kuziwezesha Timu za Afya za Mikoa 26 kufanya ufuatiliaji na usimamizi shirikishi katika halmashauri zote nchini na Shilingi bilioni 2.09 zitawezesha Ofisi ya Rais– TAMISEMI kusimamia na kutoa msaada wa kitalaam katika halmashauri na mikoa yote nchini.
Aliongeza kuwa Shilingi bilioni 5.13 zitawezesha Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kutekeleza masuala ya sera, mikakati na miongozo kwa ajili ya kuhakikisha huduma za afya zinatolewa kwa kiwango na ubora stahiki na Shilingi bilioni 8.86 zitakuwa kwa ajili ya kutekeleza maeneo mengine ya kipaumbele katika sekta.
“Vipaumbele tulivyoidhinisha na kamati ni pamoja na kutoa mafunzo kwa wataalam 620 wa dawa za usingizi; kununua machine za kisasa za kutolea dawa za usingizi katika vituo vya afya ngazi ya halmashauri na kufanya ukarabati mkubwa katika vyuo vinne (4) vya kutolea mafunzo ya watalaam wa afya”.
Prof. Mchembe alitaja maeneo mengine ya kipaumbele yaliyoidhinishwa na Kamati Kuu ya Mfuko huo kuwa ni kuhuisha Mkataba wa Makubaliano (MoU) baina ya pande zote mbili kwa kipindi cha 2021 – 2026, kununua mashine za kutolea dawa za usingizi katika vituo vya kutolea huduma za afya pamoja na kuvijengea uwezo vituo vya afya katika kusimamia na kutumia fedha kwa kuzingatia miongozo na taratibu mbalimbali.
Maazimio ya uwekaji saini Hati hiyo yamefanyika kwenye ofisi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto iliyoko mji wa Serikali Mtumba ambapo yalihudhuriwa na watalaam kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Wizara ya Fedha na Mipango, OR–TAMISEMI, Bohari ya Dawa na Wadau wa Maendeleo wanaochangia Mfuko huo kutoka Canada, Denmark, KOICA, Ireland, Switzerland, UNICEF, UNFPA na Benki ya Dunia. walioshiriki kwa njia ya ‘video conference’.
Chanzo: issamichuzi.blogspot.com
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.