Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto iko mbioni kuanzisha huduma shikizi za tiba ya methadone kwa waathirika wa madawa ya kulevya ya Heroine.
Hayo yamesemwa na Dkt. Erasmus Mndeme Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Rufaa ya Kitaifa ya Magonjwa ya Akili - Milembe alipokuwa akiwasilisha taarifa ya huduma za tiba kwa waathirika wa madawa ya kulevya kupitia dawa ya Methadone na utekelezaji wa majukumu ya Kituo cha kuhudumia waathirika wa madawa ya kulevya cha Itega Jijini Dodoma kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi na Madawa ya Kulevya walipofanya ziara ya ukaguzi wa huduma katika Kituo hicho wiki iliyopita.
“Kumekuwa na msongamano mkubwa katika maeneo yanayotoa huduma za Methadone kwenye Jiji la Dar Es Salaam ambapo kwa sasa kwenye kliniki zote tatu idadi ya wagonja imeongezeka maradufu” anabainisha Dkt. Mndeme
Amesema kuwa hali hiyo imechagiza waratibu wa huduma hizo katika ngazi ya Taifa kufikiria mbinu mbadala ya kuboresha huduma hizo nchini.
“Mojawapo ya mbinu zilizokubalika katika kukabiliana na changamoto hii ni uanzishwaji wa satellite kliniki nne kwenye ngazi ya Halmashauri na kituo kimoja kwenye gereza la Seregea ifikapo 2020” amesema Dkt. Mndeme.
Dkt. Mndeme amesema kuwa mkakati wa uanzishwaji wa Satellite kliniki unalenga kupunguza msongamano kwenye kliniki na kutoa mwanya kwa watoa huduma kuwa na muda zaidi wa kuwaona wagonjwa na kuwapa huduma stahiki.
Amesema kuwa kupeleka huduma kwenye Halmashauri itasaida waathirika kupata huduma karibu na makazi yao.
Hata hivyo Dkt. Mndeme amesema kuwa Serikali imeandaa mkakati wa awamu ya pili ya upatikanaji wa huduma za kutoa dawa kwa waathirika “Methadone” kwa mwaka 2019-2020 huku huduma zikisogezwa kwenye mikoa ya Tanga, Pwani, Morogoro, Dodoma, Arusha na Kilimanjaro huku huduma zikiwa zimeanza kutolewa kwenye mikoa ya Dodoma na Pwani.
Aidha kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kuduma ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi na Madawa ya Kulevya Mhe. Oscar Mukasa ameonyesha kufurahishwa na mkakati huo ambao utasaidia upatikanaji wa huduma kwa waraibu wa madawa ya kulevya na kuwataka wataalam kuongeza nguvu katika mapambano ya madwa ya kulevya na magonjwa ya kuambukiza baina ya waathirika wa madawa ya kulevya yakiwemo maambukizi ya Virusi vya Ukimwi na ugonjwa wa kifua kikuuna na homa ya ini miongoni mwa waathirika wa madawa ya kulevya.
Dkt. Erasmus Mndeme Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Magonjwa ya Akili - Milembe alipokuwa akiwasilisha taarifa yake kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya masuala ya Ukimwi na Madawa ya Kulevya (hawapo pichani)
Chanzo: afyablog.moh.go.tz
Habari zaidi: Serikali kuendelea kuboresha huduma za Methadone nchini
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.