SERIKALI kwa kushirikiana na wadau itajielekeza kutekeleza mpango wa kudhibiti tatizo la watoto kukimbilia mtaani kwa kufanyia kazi sababu zinazowafanya kufika mitaani badala ya kusubiri waingie mitaani na kuanza kuwakusanya ili kuwalea katika Makao ya watoto.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ameyasema hayo alipojumuika kula chakula cha Sikukuu ya Pasaka na baadhi ya watoto wanaotunzwa katika Makao ya kulelea watoto Kurasini na SOS Village, Dar es salaam.
Amesema lengo ni kushughulikia changamoto zinazowafanya watoto kushindwa kupata malezi ikiwemo migogoro ya familia na mazingira yoyote hatarishi.
"Hata hivyo, tunahitaji kupata taarifa za mlikotokea na historia ya maisha yenu kwani tunahitaji kuzuia watoto kukimbilia mitaani na serikali ndiyo ianze kuwachukua tena kutoka mitaani kwa gharama kubwa kuwapeleka kwenye vituo vya kulea watoto"
Waziri Dkt. Gwajima ameongeza kwamba, ni muhimu kuwa na mfumo ambapo wazazi, walezi na Serikali watakuwa na mawasiliano ya taarifa za mapema kuhusu watoto wenye uhitaji na walio kwenye hatari ya kushindwa kuishi majumbani ili changamoto zao zipatiwe majibu mapema kabla mtoto hajakimbia kwenda mtaani au apewe rufaa kwenda vituo salama kabla ya kuingia mitaani.
"Mtoto mdogo kuishi mtaani peke yake hata kama ni muda mfupi kiasi gani ni hatari na hasara kubwa. Lazima tuzuie na tutafanya mjadala na OR TAMISEMI kuimarisha kuzuia zaidi kuliko kujibu"
Aidha, amewataka watoto wote nchini kuzingatia masomo yao na kuwasihi watoto wanaolelewa kwenye Makao kutumia fursa waliyoipata kutimiza ndoto zao.
Kwa upande wao baadhi ya vijana waliopita katika malezi ya Makao wameipongeza Serikali kwa jitihada inazofanya kuhakikisha watoto wote wanakuwa katika misingi imara.
"Nawasihi wazazi waendelee kuwalea watoto wao bila kuwaacha Ili wasipate changamoto ya malezi" amesema Innocent Suta.
Naye Mratibu wa malezi katika shirika la SOS Village Emmanuel Mwende ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii kwa ushirikiano kwa wadau wanaotunzwa watoto.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.