WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Innocent Bashungwa amesema Serikali itatumia kiasi cha shilingi trioni 2. 78 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya elimu nchini.
Ameyasema hayo juzi tarehe 24 Septemba, 2022 jijini Arusha wakati akitoa taarifa kwa umma kuhusu utekelezaji wa miradi ya elimu nchini.
Mhe Bashungwa alisema kupitia mradi wa kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) Serikali imetoa Shilingi Trilioni 1.2 kwa lengo la kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu ya Sekondari, kuweka mazingira salama kwa wasichana waliopo katika shule za Sekondari, na kuhakikisha wanafunzi wote wanamaliza elimu ya Sekondari na kufikia malengo yao.
Bashungwa alifafanua kuwa Mradi wa Kuboresha Elimu ya Awali na Msingi (BOOST): Utatoa Shilingi Shilingi Trilioni 1.15. ambapo utaboresha mazingira ya kujifunzia katika shule za umma kwa kujenga miundombinu ya elimu, kuimarisha umahiri wa walimu na ubora wa ufundishaji darasani, kwa kutoa mafunzo endelevu ya walimu kazini.
Programu ya Kutekeleza Elimu kwa Matokeo awamu ya Pili (EP4R II) itatoa Shilingi bilioni 435.90 kwa lengo la kuendelea kujenga miundombinu mbalimbali ya shule yaani madarasa, vyoo, mabweni na nyumba za walimu, pamoja na kununua vifaa vya kufundishia.
Alieleza kuwa afua zitakazotekelezwa ni pamoja Ujenzi wa Vyumba vya madarasa, Ujenzi wa Nyumba za Walimu, Ujenzi wa Maktaba, Ujenzi wa Matundu ya Vyoo, Ujenzi wa Mabweni, Ujenzi wa Mabwalo, Ujenzi wa Maabara, Ujenzi wa vyumba vya TEHAMA, Kutoa mafunzo endelevu kwa walimu kazini, na Ununuzi wa Vifaa vya TEHAMA.
Aidha Waziri Bashungwa amewaagiza Wakuu wa Mikoa wote nchini kuhakikisha wanafuatilia miradi yote ya Maendeleo ambayo fedha zake zipo kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa na inakamilishwa iifikapo tarehe 31 Oktoba, 2022 na wakurugenzi watakaoshindwa kukamilisha miradi ya Maendeleo ifikapo tarehe hiyo taarifa itolewe ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi yao.
Pia amewataka wakuu hao wa Mikoa kuhakikisha wanawasimamia Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa ufanya matumizi sahihi ya fedha zote za miradi kwa kufuata Miongozo inayotolewa juu ya fedha hizo ili kupata thamani halisi ya fedha hizo kwa miradi inayotekelezwa.
Bashungwa ameelekeza kuhakikisha ufuatiliaji wa karibu wa ujenzi wa miundombinu ya miradi ya maendeleo wanayoletewa ili kuepuka hoja za ukaguzi zisizo za lazima.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.