NAIBU Waziri wa Kilimo Mhe. Anthony Mavunde amesema serikali ipo njiani kutunga sheria maalum kwa ajili ya kilimo ili kulinda maeneo yote yanayofaa kwa kilimo katika azma yake ya kukuza sekta ya kilimo nchini.
Mheshimiwa Mavunde ameyasema hayo jana wakati akizungumza na wananchi wa kata ya Ihusi - Bariadi, Mkoani Simiyu katika mkutano wa hadhara wakati kamati ya mawaziri 8 wa kisekta wanaoshughulikia migogoro ya ardhi ya Vijiji 975 walipofika katika eneo hilo.
“Katika kulinda maeneo yanayofaa kwa kilimo na kupunguza migogoro ya matumizi ya ardhi nchini, serikali kupitia wizara ya kilimo tunaendelea na hatua za utungwaji wa sheria ya kilimo.
Kwakuwa dhamira yetu kubwa ni kuhakikisha tunakuza sekta hii ya kilimo kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030, hatua hii lazima iende sambamba na kuyatambua maeneo ya kilimo na kuyalinda kisheria.
Katika maeneo yote ya utatuzi wa migogoro hii ambapo ardhi inamegwa kwa ajili ya kuwagawia wananchi kuendelea na shughuli za uzalishaji mali, mamlaka za upangaji wa matumizi bora ya ardhi katika maeneo husika hakikisheni mnatenga maeneo ya mashamba makubwa ya pamoja ya kilimo (block farms) ili serikali iweze kuwahudumia wakulima kwa urahisi” Alisema Mavunde.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Mavunde ametoa rai kwa wakulima wote kuendelea na kukamilisha zoezi la usajili wao ili wanufaike na huduma mbalimbali kutoka serikalini na hasa mbolea ya ruzuku ambapo serikali imetenga zaidi ya Tsh 150 bilioni kama sehemu ya ruzuku ya mbolea ili kumpunguzia mzigo mkulima.
Hatua hiyo inafuatia kupanda kwa bei ya mbolea katika soko la dunia jambo linalowafanya wakulima wa kawaida kushindwa kumudu kununua mbolea na hivyo kuathiri kukua kwa uzalishaji wa mazao ya kilimo nchini.
Amesema kiasi hicho cha fedha kilichotengwa kitawawezesha wakulima kununua mbolea kwa nusu bei iliyopo kwenye soko.
NAIBU Waziri Mavunde alitumia wasaa huo pia kumshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza bajeti ya Wizara ya Kilimo kutoka Bilioni 294 hadi Bilioni 954 ambapo Shilingi Bilioni 400 zimeelekezwa katika kilimo cha umwagiliaji hasa katika kuyafanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina mabonde yote makubwa nchini sambamba na ujenzi wa mabwawa mapya 13.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.