Na. Theresia Nkwanga, TAMBUKARELI
SERIKALI ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan inatekeleza miradi mingi ya maendeleo kwa lengo la kuwaletea maendeleo wananchi wa Kata ya Tambukareli.
Kauli hiyo ilitolewa na Diwani wa Viti Maalum Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Leticia Sanga alipokuwa akiongea na wananchi wa kata ya Tambukareli katika ziara ya madiwani wa viti maalum wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kuwahamasisha wananchi waliokopa kurejesha mikopo ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Sanga alisema kuwa serikali ya Awamu ya Sita imepeleka fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo Dodoma na hasa katika kata ya Tambukareli. “Wananchi wote tunaona mama yetu Samia Suluhu Hassan anavyojenga shule, zahanati na barabara. Nafikiri mnaona kila mahali kuna shule nzuri na barabara nzuri, Anajenga zahanati na hospitali nzuri ili tukiugua tukahudumiwe vizuri, tukitaka kujifungua tujifungue salama. Vilevile, nimpongeze sana Rais kwa kuzindua Ikulu hapa Dodoma, maana yake makao makuu ya Tanzania ni rasmi Dodoma” alisema Sanga.
Aidha, alimshukuru kwa utekelezaji miradi ya kitaifa. “Tunamshukuru mama Samia kuendeleza miradi yote iliyoanzishwa na mwenda zake Rais, Dkt. John Magufuli mfano miradi ya barabara ya mzunguko Dodoma, Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Msalato unaendelea. Miradi mipya ambayo ameibuni mama inasimamiwa vizuri na inaendelea. Kipekee nimshukuru kaka yangu Joseph Mafuru, Mkurugenzi wetu wa Jiji la Dodoma kwa kazi nzuri anayoifanya kwa kusimamia fedha zote za miradi anazopewa na Mheshimiwa Rais ili Dodoma Jiji iweze kuwa imara na kupendeza zaidi” alisema Sanga.
Akiongelea mikopo inayotolewa na Halmashauri ya jiji kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu alisema inalenga kuwakomboa wananchi kiuchumi. “Halmashauri ya Jiji la Dodoma inatoa mikopo ya asilimia 10 kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Mikopo hii haina riba. Ni fursa kwa wananchi wetu kujikomboa kiuchumi kwa kukuza mitaji yao. Nitumie nafasi hii kuwahimiza wakopaji wote kuhakikisha mnarejesha mikopo hiyo ili iweze kunufaisha watu wengi zaidi” alisema Sanga.
Aidha, alimpongeza Diwani wa Kata ya Tambukareli, Juma Michael kwa kazi nzuri na usimamizi wa shughuli za maendeleo katika kata hiyo. “Mheshimiwa Diwani anaisemea vizuri kata hii, hivyo muendelee kumuunga mkono. Kipekee nimshukuru Mbunge wa Jimbo la Dodoma mjini kwa kazi nzuri za maendeleo anazofanya hapa Dodoma kuhakikisha miradi yote ya maendeleo inaenda vizuri” alisema Sanga.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.