SERIKALI ya Tanzania imefadhili jumla ya miradi 215 ya sayansi, teknoljia na ubunifu katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, mifugo, afya, nishati, maliasili na viwanda kuanzia mwaka 2015, ambapo miradi 139 imekuwa ya utafiti, 47 ya kiubunifu, 29 ya kuboresha miundombinu ya maabara za utafiti.
Hayo yamesemwa leo na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika kilele cha mashindano ya kitaifa ya sayansi, teknolojia na ubunifu (MAKISATU) mwaka 2021, yaliyofanyika katika uwanja wa Jamhuri jijini hapa.
Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa mashindano hayo yana umuhimu mkubwa sana katika kuboresha uchumi wa nchi. Mashindano hayo yanagusa uchumi wa mtu binafsi na kuleta mafanikio ya kiuchumi kimataifa, aliongeza.
“Lakini vilevile, kwa upande wa mitaala kutoka ngazi mbalimbali za elimu ni vyema tuandae mitaala ya namna ambayo itawafanya wahitimu kuwa wabunifu mwisho wa masomo yao” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.
Waziri Mkuu huyo ameendelea kusema kuwa kazi kubwa ni kuibua, kuinua lakini kutoa kipaumbele, na hati miliki ya mgunduzi ni kipaumbele sababu ndio njia ya kumfanya apate faida kupitia ubunifu wake.
“Takwimu zetu zinaonesha kuwa shirika la hati miliki duniani linaitwa World Intellectual Property Organisation, linalokusanya maombi ya hati miliki kutoka nchi mbalimbali mpaka kufikia mwaka 2020 kwa Tanzania tulipeleka maombi nane huku nchi za jirani 372, afrika ya kusini 1,514” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.
Aidha, ameshukuru taasisi 50 za serikali na zisizo za kiserikali zilizoshiriki katika mashindano ya kitaifa ya sayansi, teknolojia na ubunifu, na kuongeza kuwa changamoto zilizopo zimekwisha elekezwa kwa wizara na taasisi zenye dhamana.
Mashindano hayo yaliandaliwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, yamefanyika kwa mara ya tatu katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma yakiongozwa na kaulimbiu isemayo sayansi, teknolojia na ubunifu kwa uchumi endelevu.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.