Serikali chini Tanzania imeweka mpango madhubuti wa kuwawezesha vijana kushiriki kikamilifu kwenye sekta ya kilimo kwa kuwapatia ujuzi wa mbinu za kilimo bora na kuwawezesha mitaji ya kuanzia kupitia mifuko ya uwezeshaji wananchi ili kutatua changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana nchini.
Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Anthony Mavunde wakati wa ziara ya kutembelea miradi ya Vijana inayotekelezwa kupitia Programu ya Opportunities for Youth Employment (OYE) katika Kata za Kikore-Wilaya ya Kondoa na Kata ya Dareda-Babati ambapo vijana wengi wamejiajiri kupitia sekta ya kilimo na ufugaji wa samaki na hivyo kuwasaidia kutatua changamoto za kipato na kushiriki kikamilifu kwenye ujenzi wa uchumi wa Taifa.
"Serikali chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli tutaendelea kuwapa mafunzo stahiki vijana kuhusu kilimo cha kisasa na kutumia teknolojia bora. Kwa sasa tumeanza na mafunzo ya kilimo kwa vijana nchi nzima kupitia 'Greenhouse' na kuwawezesha kupitia mikopo mbalimbali ili waweze kufikia lengo na matarajio yao, na muitikio wa vijana kwa sasa umekuwa mkubwa ndio maana tunaendelea kusisitiza mamlaka za Manispaa na Wilaya kutenga maeneo maalum kwa ajili ya kilimo kwa vijana" Alisema Mavunde.
Naye Meneja Mradi wa OYE kutoka Shirika lisilo la Kiserikali la Nchini Uholanzi (SNV) Bi. Jeann Mwenda amesema kwamba Program ya OYE kwa muda wa miaka 7 tangu kuanzishwa kwake imewafikia na kubadilisha maisha ya vijana 18,000 na hivyo kuiomba Serikali kushirikiana na SNV ili kuwafikia vijana wengi zaidi nchini kuliko ilivyo hivi sasa ambapo mradi huu unatekelezwa katika mikoa michache tu.
Akizungumza kwa niaba ya vijana wengine wanufaika, kijana Marcel Damas wa Kijiji cha Bermi, Kata ya Dareda - Babati ameishukuru serikali katika ngazi ya wilaya kwa kuwasimamia vizuri mpaka kupata mafunzo na uwezeshwaji kupitia programu ya OYE na kutumia fursa hiyo kuwataka vijana wengine waache kulalamika na badala yake wafanye kazi hasa kupitia kilimo.
Baadhi ya picha za matukio aliyoshiriki Naibu Waziri Mavunde.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.