Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, TAMISEMI Mhandisi Joseph Nyamhanga amekabidhi majengo na eneo lililokuwa linamilikiwa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini - IRDP.
Akiongea katika hafla fupi ya makabidhiano ya majengo na eneo hilo lililopo katikati ya Jiji la Dodoma barabara iendayo Iringa, Mhandisi Nyamhanga amesema awali majengo hayo yalikuwa yakimilikiwa na iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) na baada ya kuvunjwa kwake yalikabidhiwa kwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma na Chuo cha Mipango walikuwa wapangaji katika majengo hayo.
“Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini kilikuwa kinapanga hapa na kilikuwa kinalipa gharama kubwa, naambiwa zaidi ya shilingi milioni 250 kwa mwaka kwa ajili ya wanafunzi kusoma, lakini sasa Serikali imeamua kwamba hosteli hii ikabidhiwe kwa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini kilichopo Jijini Dodoma”.
Makabidhiano hayo yamefanyika leo kwa kubadilishana hati kati ya Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhandisi Joseph Nyamhanga kwa niaba ya Serikali na Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo ya Vijijini Profesa Hozen Mayaya.
Mhandisi Nyamhanga amemtaka Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini kukarabati majengo hayo lakini pia kuondoa majengo ya muda yaliyokuwa yakitumiwa kama madarasa na kujenga majengo mapya ya kudumu kwa kuwa sasa hawapangi tena na wao ndio wamiliki.
Amewataka wanafunzi wote wa chuo hicho kusoma kwa bidii na kuinua kiwango cha ufaulu. Nyamhanga amemshukuru Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ambaye amekuwa mstari mbele na kufanya jitihada kubwa za kuboresha elimu kuanzia shule za awali, msingi, sekondari, vyuo vya ufundi na vyuo vikuu nchini.
Kwa upande wake Mkuu wa chuo cha Mipango Profesa Hozen Mayaya ameishukuru Serikali kwa maamuzi mazuri ya kuwakabidhi majengo hayo na eneo ambalo litasaidia kuboresha miundombinu na mazingira rafiki ya kujifunzia kwani gharama za upangaji katika majengo hayo zilikuwa kubwa ambazo ni zaidi ya milioni 252 kwa mwaka.
Aidha, Mayaya alisema Chuo cha Mipango bado kina uhitaji wa miundombinu ya majengo ya madarasa na hosteli kutokana na kudahili wanafunzi wengi kutoka mikoa karibu yote hapa nchini.
Katika makabidhiano hayo Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma aliwakilishwa na Elihuruma Mufuruki, Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi wa Jiji la Dodoma.
Chanzo: Tovuti ya tamisemi.go.tz
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.