WANANCHI wametakiwa kuzingatia usafi binafsi wa mwili na mikono kwa kutumia maji safi tiririka na sabuni mara kwa mara katika maeneo yote ikiwemo maeneo ya kazi, mashuleni, vyuoni, nyumba za ibada, baada ya kutoka maliwatoni na mazingira yenye uchafu.
Rai Imetolewa na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi Jijini Dodoma wakati akitoa tamko la wiki ya Elimu ya Afya kwa Umma kwa ajili ya kuimarisha udhibiti wa magonjwa yanayoambukiza na yasiyoambukiza.
Prof. Makubi amesema kuwa wananchi wanapaswa kufahamu kuwa kinga ni bora kuliko tiba kwani tiba ni gharama na siyo lazima upone maana inaweza kusababisha kifo au ulemavu wa kudumu pamoja na maradhi mengi ikiwemo ya kuambukiza na yasiyoambukiza ambayo yanazuilika iwapo kila mmoja atapata elimu juu ya magonjwa haya na jinsi ya kuzuia.
Aidha, amesema mkakati wa utekelezaji wa usafi umeleta matokeo chanya kwa kipindi cha miaka mwili iliyopita hadi sasa ambapo nchi haijapata visa vya kipindupindu.
“Sasa ni vema kuhamasisha jamii iendelee na hii tabia ya kuhakikisha vifaa vya kunawia na sabuni vinakuwepo katika maeneo yote kuanzia nyumbani hadi mahala pa kazi na ambapo watu hukusanyika ili tuzidi kujikinga na magonjwa yote ya kuambukiza kupitia uchafu ikiwemo magonjwa ya kuhara na mafua”. Alisisitiza Prof. Makubi.
Kuhusu usafi wa mazingira Prof. Makubi alisema wananchi wahakikishe nyumba zinakuwa safi na mizunguko ya hewa inakuwepo ili kujikinga dhidi ya magonjwa ya mafua, homa ya mapafu, malaria, kifua kikuu na ili kulinda kinga za mwili zisishambuliwe na maradhi mara kwa mara. Wananchi wanatakiwa kula lishe bora ili kuimarisha kinga za mwili kwa kula vyakula visivyo na sukari nyingi, kula matunda na kunywa maji kadri ya mahitaji ya mwili.
Hata hivyo Prof. Makubi alihimiza kuwa ufanyaji wa mazoezi ya mwili na viungo ni nguzo muhimu katika kujenga nguvu za mwili ili kuimarisha mifumo ya hewa, mapafu na moyo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.