Na. Prisca Maduhu, CHIHANGA
SERIKALI ya awamu ya sita imepeleka miradi mingi ya maendeleo katika Kata ya Chihanga ikiwa ni pamoja na umeme jambo lililorudisha nuru kwa wananchi.
Kauli hiyo ilitolewa na Diwani wa Kata ya Chihanga, Elisi Chitendya alipokuwa akishukuru baada ya Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Dodoma kufanya ziara ya kutembelea miradi ya maendeleo katika kata hiyo.
Chitendya alisema “Kata ya Chihanga ni miongoni mwa kata zinazopendelewa na viongozi wa serikali. Kwenye Baraza la Madiwani nikiomba miradi nasikilizwa na ninapewa miradi. Aidha, serikali kuu pia imeleta miradi mingi ya maendeleo ambayo Rais, Mama Samia Suluhu Hassan anatutekelezea. Wananchi wa Chihanga wanaipenda sana CCM”.
Chitendya alisema kuwa tangu kuumbwa kwa ulimwengu, kata yake haikuwa na umeme, serikali ya awamu ya sita imepeleka umeme. “Napenda kumshukuru sana Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametuona wananchi wa Kata ya Chihanga. Tulikuwa na changamoto ya watumishi, sasa tuna watumishi wa kutosha. Mfano nilikuwa na watendaji mitaa wawili kati ya mitaa nane. Kwenye ajira mpya, nimefanikiwa kupata watendaji wa mitaa watano. Tulikuwa na shida sana ya walimu wakikaa mjini lakini serikali imetuona, tumeletewa fedha na tunajenga nyumba za walimu sasa” alisema Chitendya.
Akielezea furaha ya wananchi wake kwa serikali yao, alisema kuwa imerudisha matumaini. “Kuna Mtaa wa Sogeambele ambao ulisahaulika kabisa, hakuna Mbunge wa Jimbo la Dodoma aliyewahi kufika. Lakini Mbunge Anthony Mavunde alifika na wananchi walieleza changamoto zao na waliomba umeme, barabara, maji na zahanati. Na katika miradi hiyo minne, miradi mitatu imeanza kutekelezwa na mradi ambao bado ni wa umeme ambao bajeti itatoka wakati wowote sababu mama Samia anapenda wananchi wake na umeme utakuja” alisema Chitendya kwa kujiamini.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.