SERIKALI imewapongeza watawa wanaosimamia watoto yatima wa kituo cha Nyumba ya Matumaini kilichopo Kata ya Miyuji Halmashauri ya jiji la Dodoma kwa kazi ya kulea watoto hao.
Pongezi hizo zilitolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Madhimisho ya siku ya Wanawake katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Hildagrace Makwinya hivi karibuni katika kituo hicho.
Makwinya alisema “napenda kuwapongeza sana watawa wanaolea watoto hawa katika kituo hiki cha nyumba ya Matumaini, pongezi kwa kazi ya ulezi mliyonayo, hakika ninyi ni kina mama na kina baba kwa hawa watoto kazi mnayofanya ni nzuri na kubwa”, aliongeza.
Akiongelea changamoto inayowakabili watoto wa kituo hicho ya kutokuwa na vyeti vya kuzaliwa alisema, serikali italishughulikia suala hilo.
“Nimepokea tatizo la watoto wengi katika kituo hiki cha nyumba ya Matumaini kutokuwa na vyeti vya kuzaliwa jambo linalosababisha watoto hawa wakose baadhi ya huduma muhimu. Bahati nzuri wizara yetu ya Sheria na Katiba ndiyo inahusika na usajili huo” alisema Makwinya.
“Nitawasiliana na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) ili kuhakikisha watoto hawa wanasajiliwa na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa kwa mujibu wa taratibu” aliongeza.
Naye Mkuu wa idara ya Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Sharifa Nabalang’anya alisema kuwa, jukumu la kulea watoto ni zito na linalohitaji uwajibikaji wa pamoja.
“Hakika mnafanya kazi ya Mungu, napenda kuwatia moyo japo kuna changamoto ila malipo yenu ya uhakika ni mbinguni…Serikali ipo pamoja nanyi na nichukue nafasi hii kuwakaribisha katika katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji mnapokuwa na changamoto zinazohitaji utatuzi wa pamoja ili tushirikiane katika kuzitatua” alisema Nabalang’anya.
Nae mkuu wa msafara huo ambaye pia ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Jinsia katika Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Grace Mwangwa aliwaomba kuendelea na moyo huo thabiti wa kuwalea watoto hao.
“Wizara inawashukuru sana na inawaunga mkono, ustawi wa watoto ni kipaombele cha Wizara” alisema Mwangwa.
“Maadhimisho ya siku ya Wanawake huambatana na shughuli mbalimbali, hivyo siku ya leo ni mahususi kwa ajili ya kutembelea maeneo ya watu wenye mahitaji maalum…watatembelewa wafungwa katika Magereza, vituo vya kulelea Wazee, watu wenye ulemavu na watoto yatima” aliongeza.
Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamaii, Jinsia, Wazee na Watoto- Idara ya Ustawi wa Jamii, Verediana Kimaro alisema kuwa wizara kwa kushirikiana na wadau imeanza utaratibu wa kutoa bima za afya kwa vituo vya kulelea watoto.
“Tunataka watoto wote wawe na bima ya afya” alisema Kimaro.
Awali akitoa taarifaf upi ya kituo hicho, msimamizi wa kituo Sr. Aurea Kyara alisema kuwa kituo hicho kina watoto 63 wenye umri kuazia miaka mitatu hadi saba. Alisema kuwa watoto hao wanakabiliwa na changamoto ya bima kwa ajili ya matibabu, vyeti vya kuzaliwa na shule wanazosoma kuwa mbali na kituo hicho.
Aidha, aliyataja mafanikio ya kituo kuwa ni baadhi ya watoto waliolelewa kituoni hapo kufikia hatua ya Vyuo na Vyuo Vikuu.
Mengine ni Mkoa kufanikisha baadhi ya watoto kupata vyeti vya kuzaliwa na jamii inayozunguka kituo kutoa ushirikiano mzuri.
Timu ya kima mama kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamaii, Jinsia, Wazee na Watoto, Wizara ya Sheria na Katiba, Halmashauri ya Jiji la Dodoma na wadau kutoka taasisi mbalimbali walipeleka zawadi kituoni hapo zikiwemo taulo za kike, sukari, sabuni, mafuta ya kula na kupaka, mikate, nguo, dawa za meno, dawa za kuulia mbu, pipi pamoja na vitu vingine.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.