SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepongezwa kwa kujali elimu jumuishi katika shule za awali na msingi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma na kutoa fursa kwa watoto wengi kusoma.
Pongezi hizo zilitolewa na Mkuu wa Divisheni ya Awali na Msingi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwl. Prisca Myalla alipoongoza zoezi la kutoa kadi za bima za afya na vifaa kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum katika Shule ya Msingi Mlezi iliyopo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Mwl. Myalla alisema “siku ya leo ni siku jumuishi ya kuhimiza elimu jumuishi kwenye shule zetu. Tunamshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan anaendelea kulisimamia hilo kwenye shule zetu kama ambavyo leo tumekusanyika hapa kugawa vifaa kwa wanafunzi wetu wenye mahitaji maalum kwa shule nane zilizopo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma. Tunaona kabisa ana nia ya dhati kuhakikisha na watoto wetu wenye mahitaji maalum wanapata elimu iliyo sawa na watoto ambao hawana mahitaji maalum”.
Alisema kuwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeandaa kadi za bima za afya 49 kati ya 100 kwa ajili ya kupata huduma za kiafya kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum. “Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa imeandaa vifaa vya kufundishia na kujifunzia ili nao wapate elimu iliyo bora kwa watoto wetu wenye mahitaji maalum kupitia shule zetu zilizopo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma. Tunawashukuru wadau kwa kutoa vitimwendo kwa wanafunzi wetu wenye ulemavu. Tunatarajia wadau wa namna hii kuendelea kuiunga mkono halmashauri yetu. Huu ndiyo ushirikiano wa taasisi binafisi na serikali katika kuunga mkono maendeleo ya nchi yetu kupitia elimu” aliongeza Mwl. Myalla.
Akisoma taarifa fupi ya elimu maalum, Mkuu wa seksheni ya Elimu Maalum, Mwl. Issa Kambi alisema “tunaishukuru serikali ya awamu ya sita, kupitia Ofisi ya Rais, Tamisemi kwa kutenga kwenye bajeti ya mwaka 2023/2024 jumla ya shilingi 323,366,172 kwa ajili ya chakula cha wanafunzi wenye mahitaji maalum. Kila mwezi tunapokea jumla ya shilingi 26,947,181 kupitia ruzuku zinazoingizwa katika shule zenye wanafunzi wenye mahitaji maalum”.
Alisema kuwa katika bajeti ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma kupitia fedha za uendeshaji imetenga jumla ya shilingi 26,460,000 kwa ajili ya shughuli mbalimbali na ununuzi wa vifaa visaidizi na vifaa vya kufundishia na kujifunzia wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Akiongea kwa niaba ya maafisa elimu kata wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Afisa Elimu Kata ya Hazina, Mwl. Zaituni Mkoyi alisema “kwa niaba ya maafisa elimu kata wa shule hizi nane ambazo tumekutana hapa, naishukuru serikali na wizara zake kuona umuhimu na kuwajali watoto hawa ambao ni kundi maalum. Nipongeze wazazi kuendelea kuwaleta watoto ili waweze kupata elimu ambayo ni haki yao. Niombe muwe chachu na ushawishi kwa wazazi wengine ambao bado wanaendelea kuwaficha watoto kama hawa”.
Mzazi wa mwanafunzi mwenye mahitaji maalum, Hincha Kweji alisema kuwa walimu wanaofundisha watoto wenye mahitaji maalum wanaupendo mkubwa. “Walimu hawa wamekuwa ni elimu kubwa sana kiasi kwamba wazazi tumefika mahali tukawapenda watoto wetu, ina maana walimu wametufundisha kuwapenda watoto wetu wenye mahitaji maalum” alisema Kweji.
Ikumbukwe kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoam ina jumla ya shule 61 zinazopokea watoto wenye mahitaji maalum, kati ya shule hizo 10 ni vitengo vya watoto wenye mahitaji maalum na moja ni maalum na shule 50 ni jumuishi. Jiji likiwa na wanafunzi 1,056 wenye mahitaji maalum.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.