Na. Asila Twaha, Dodoma
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameridhishwa na ujenzi wa jengo la Ofisi ya Rais - TAMISEMI na kuwaasa watendaji wa wizara hiyo kuendelea kusimamia kasi ya ujenzi wake ambalo tayari limefikia asilimia 54.
Majaliwa ametoa wito huo mapema leo Jijini Dodoma baada ya kupokea taarifa ya ujenzi na kukagua jengo hilo ambalo Serikali imetoa fedha kwa ajili ya muendelezo wa ujenzi wa Ofisi za Wizara zote za Serikali.
Amewapongeza mafundi na mkandarasi na kuwataka viongozi na watendaji wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI kuendelea kushirikiana na mkandarasi na mafundi ili kufikia lengo la Serikali la kujenga Ofisi zote za wizara hiyo katika Mji wa Serikali Mtumba.
“ Niwapongeze mafundi, taarifa inaonesha asilimia ya ukamilishaji ipo juu kuliko ilivyo kadiriwa”
Majaliwa amesema, azma ya Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ni kuendelea na kuuendeleza Mji wa Serikali pamoja na Makao Makuu ya Nchi, Jijini Dodoma kwa kujenga miundombinu ya barabara, miundombinu ya mifumo ya maji na kuendelea na ujenzi wa Wizara za Serikali ambapo zaidi ya bilioni 500 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa Wizara za Serikali lakini pia uwekezaji uliowekwa kwa kuendelezwa Dodoma.
Awali akisoma taarifa ya maendeleo ya ujenzi Mkurugenzi wa Maendeleo ya Miundombinu Ofisi ya Rais, TAMISEMI Mhandisi Gilbert Moga amesema, kwa mujibu wa kazi zilizotakiwa kukamilika hadi kufikia Agosti 30, 2022 ni umwagaji wa zege kwenye nguzo, ngazi na kuta kutoka kitako cha chini hadi sakafu ya pili ambayo ni asilimia 19.
Mhandisi Moga amesema hadi Septemba 5, 2022 hatua iliyofikiwa ni asilimia 54 ya mpango kazi ambapo Mkandarasi yupo mbele kwa asilimia 35.
Majaliwa amesema, ziara hiyo ni muendelezo wa kukagua ujenzi wa Makao Makuu ya Nchi ambapo alianza kwa kukagua ujenzi wa barabara ya mzunguko na kwamba ataendelea kukagua na kuona ujenzi wa majengo ya wizara mbalimbali yanayoendelea kujengwa ili kujiridhisha na maendeleo yake.
Ujenzi wa jengo la Ofisi ya Rais, TAMISEMI unaoendelea kujengwa Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma unasimamiwa na Mtaalam Mshauri kutoka kwa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA)
Chanzo: Tamisemi
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.