WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema ndani ya mwaka mmoja, Serikali imefanikiwa kusajili miradi 9,678 yenye thamani ya dola za Marekani milioni 8,658 hali ambayo inaonesha matokeo chanya ya uwekezaji nchini.
“Miradi 9,678 yenye thamani ya dola za Marekani milioni 8,658 ilisajiliwa mwaka 2023 ikilinganishwa na miradi 8,401 yenye thamani ya dola za Marekani milioni 5,558.47 iliyosajiliwa mwaka 2022,” amesema.
Alitoa kauli hiyo jana usiku (Jumatano, Septemba 11, 2024) wakati akizungumza na wadau mbalimbali walioshiriki hafla ya uzinduzi wa Taarifa tano za Maboresho ya Mazingira ya Biashara na Uwekezaji na Nyenzo za Usimamizi wa Uwekezaji nchini iliyofanyika kwenye ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
Akifafanua kuhusu taarifa ya kwanza ya uwekezaji ya mwaka 2023 ambayo inaonesha takwimu za matokeo chanya ya uwekezaji nchini, Waziri Mkuu alisema miradi hiyo imeweza kuzalisha ajira za moja kwa moja 195,803 ikilinganishwa na ajira 76,841 zilizozalishwa mwaka 2022.
Akielezea juhudi zilizofanywa na Serikali kwenye mipango ya maendeleo ya uwekezaji wa sekta ya umma na sekta binafsi, pamoja na mazingira ya biashara, Waziri Mkuu alisema Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kufanya mageuzi ya uendeshaji na usimamizi wa Taasisi na Mashirika ya Umma ili kuhakikisha kwamba yanaendeshwa kwa ufanisi na tija katika kuwahudumia wananchi.
“Suala hili tayari limetolewa maelekezo na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 28 Agosti, 2024 katika kikao kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Mashirika ya Umma na Taasisi za Serikali. Hivi sasa, Serikali imeridhia mapendekezo ya kutungwa kwa Sheria ya Uwekezaji wa Umma itakayoimarisha na kuweka masharti bora ya usimamizi wa uwekezaji katika Mashirika ya Umma pamoja na kuwa na vyanzo vya uhakika vya fedha kwa ajili ya uwekezaji.”
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.