Serikali kwa kupitia Wizara ya Kilimo imepanga kujenga vituo vitatu (Storage Facilities) vya kukusanya, kuchakata na kuhifadhi mvinyo ghafi wa zabibu mkoani Dodoma kwa lengo la kuokoa zabibu za wakulima zinazooza shambani kwa kukosa masoko kwa wakati.
Hayo yamesemwa leo Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Kilimo Mh. Anthony Mavunde katika kikao cha wadau wa zabibu kilichofanyika katika ukumbi wa PSSSF Jijini Dodoma ambacho lengo lake kubwa ni kujadili muongozo wa usimamizi wa zao la zabibu kufuatia hatua inayoendelea ya uazishwaji wa Chama kikuu cha Ushirika wa wakulima wa zabibu.
“Changamoto kubwa inayowakabili wakulima wa zabibu ni kukosekana kwa soko la uhakika jambo ambalo hupelekea mkulima kuuza zabibu zake kwa bei ya hasara.
Uanzishwaji wa vituo hivyo cha uchakataji na uhifadhi wa mchuzi wa zabibu utampa uhakika mkulima kutopoteza mazao yake ya shambani kwa kuoza na hivyo kupelekea kuuza zabibu kwa bei ya chini kwakuwa sasa ataweza kuuza mvinyo ghafi utakaohifadhiwa kusubiri soko.
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuwainua wakulima wakiwemo wa zabibu kwa kukipa Kilimo kipaumbele cha juu, dhamira hii inaonekana kwa namna ambavyo bajeti ya kilimo imekwenda juu kutoka shilingi Bilioni 294 mpaka kufikia shilingi Bilioni 751.
Katika kuhakikisha wakulima wa zabibu wanazalisha kwa tija na weledi Serikali itasimamia mafunzo ya wataalam na wakulima juu ya zao la zabibu na ikiwezekana kwenda kujifunza katika nchi zinazofanya vizuri kwenye kilimo cha zabibu ili wakulima watakaopata fursa ya kujifunza wakasaidie kufundisha wakulima wengine” Alisema Mhe. Mavunde.
Wakati huo huo Mhe. Mavunde amewataka wadau wa zabibu kujadili kwa uwazi muongozo wa uzalishaji, masoko na uchakataji wa zabibu ili yapatikane mawazo yenye nia ya kujenga na hatimaye kuleta maendeleo kwenye zao hilo.
Awali akitoa salamu za mkoa wa Dodoma kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Anthony Mtaka, Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mhe. Mwanahamisi Mukunda amesema ana imani kubwa na uwezo wa Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe pamoja Naibu Waziri Mhe. Anthony Mavunde katika kuwasaidia wakulima wa zabibu mkoani Dodoma.
Aliongeza kuwa, kwa kasi ya viongozi hao pamoja na dhamira ya Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan changamoto za wakulima wa zabibu zitatatuliwa.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.