Serikali itaendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya mirathi na uandishi wa wosia ili kuondoa migogoro inayowakabili wajane nchini kutokana na kudhulumiwa haki zao.
Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile alipokuwa akiwahutubia mamia ya wananchi katika maadhimisho ya siku ya wajane duniani iliyofanyika kitaifa katika uwanja wa Nyerere square jijini Dodoma jana.
Dkt. Ndugulile alisema “sisi kama serikali kupitia Idara kuu ya Maendeleo ya jamii na wadau wote tuendelee kutoa elimu kwa jamii hususani masuala yanayohusu mirathi na kuacha wosia. Watu wengi hawajui haki zao, wanakutana huko wanaishi pamoja hakuna cheti”. Watu wote wenye ndoa za asili wasajiri ndoa hizo na kupatiwa hati za usajili, alishauri.
Aidha, wadau na taasisi nyingine ambazo zinatoa ushauri wa kisheria wametakiwa kwenda kutoa elimu kwa jamii juu ya masuala ya mirathi. “Twende tukatoe elimu kwenye jamii kuhusiana na taratibu za mirathi, nini unachotakiwa kufanya wewe mjane, badala ya kukimbilia kulia kwa uchungu, huku nyuma watu wanakuzunguka, wanaanza kutafuta hati za nyumba, wanaenda kuchukua cheti cha kifo wanaenda kukimbilia nyaraka zote nyeti ambazo mwisho wa siku zitakuja kukupa shida katika kusimamia mirathi yako” alisema Dkt. Ndugulile.
Akiongelea maadhimisho hayo, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara kuu ya Maendeleo ya jamii, Dkt. John Jingo alisema kuwa maadhimisho hayo yamewakutanisha wajane kutoka karibu mikoa yote Tanzania na Wizara yake imewajengea uwezo kuhusu masuala ya ujasiriamali na stadi za maisha.
Maadhimisho ya siku ya wajane duniani yamefanyika kitaifa kwa mara ya kwanza nchini katika jiji la Dodoma wakati dunia ikikadiliwa kuwa na zaidi ya wajane milioni 258. Kati ya wajane 10, mjane mmoja anaishi katika umasikini wa kutupwa.
Mkazi wa Mkoa wa Mwanza, Veronica Nyabumera aliiomba serikali kusaidia uanzishaji wa Sera ya taifa ya wajane itakayowatambua wajane kama kundi maalum katika jamii. Kuanzishwa kwa sera ya Taifa kwa ajili ya wajane kutasaidia kutoa msukumo kwa jamii juu ya haki na madhira wanayopitia wajane, aliongeza. Alisema kuwa kundi hilo limekuwa likidhurumiwa mali pindi wenzi wao wanapofariki. Aidha, Nyabumera alishauri kuwa vifo vya wanaume vitambuliwe kuwa vinatokana na mapenzi ya Mungu kama vilivyo vifo vya wanawake. “Pendekezo langu vifo vya wanaume navyo vitambuliwe kuwa vinatokana na mapenzi ya Mungu kama vilivyo vifo vya wanawake na siyo kurogwa. Jambo hilo ndilo linalosababisha wajane tunakosa haki zetu baada ya kufiwa na waume zetu” alisema Nyabumera kwa uchungu.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile (katikati mwenye kaunda suti) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa serikali, dini na baadhi ya wawakilishi wa wanawake wajane nchini
Naibu Waziri Ndugulile akifurahia baadhi ya bidhaa zinazotengenezwa na wanawake wajane.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.