SERIKALI imetoa zaidi ya Sh milioni 600 kwa ajili ya kujenga vituo viwili vya afya pembeni ya Barabara ya Dodoma Iringa kwa ajili ya kusaidia wananchi wa maeneo hayo na wasafari wanaotumia barabara hiyo katika wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma.
Taarifa ya ujenzi wa vituo hivyo katika kata ya Mtera na Kata ya Chipogoro wilayani humo ilitolewa kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge wakati akiwa katika ziara ya kukagua ujenzi na ukamilishaji wa vituo hivyo ili vianze kutoa huduma.
Akitoa taarifa ya Kituo cha Afya cha Mtera, Mganga Mfawidhi wa Kituo hicho, Getrudi Anase alisema Kituo cha Mtera kimejengwa kwa msaada wa serikali ya awamu ya tano ya Rais John Magufuli ambaye Aprili mwaka jana alipota hapo na akaona majengo ya kambi wakandarasi waliokuwa wakijenga barabara na kubadili matumizi na kukifanya kituo cha afya.
Getrudi alisema baada ya agizo hilo, ili majengo hayo kukidhi mahitaji, serikali ilitoa sh milioni 400 ili kuongeza miundombinu mingine ili kituo hicho kiweze kutoa huduma bora kwa wenyeji na hata wasafiri wanaotumia njia hiyo.
Katika kuoneshwa kuguswa na mchango wa serikali, wananchi wa eneo hilo walichangia sh milioni 3.6 ambazo zinatokana na kusafisha eneo, kukusanya mawe na mchanga ili kuwezesha ujenzi wa majengo matano.
Majengo yaliyojengwa na yamefikia hatua mbalimbali katika kituo hicho ni pamoja na wodi ya wazazi, jengo la upasuaji, jengo la maabara, jengo la mionzi na jengo la kuhifadhia maiti.
Hadi kufikia Agosti 30, mwaka huu fedha zilizotumika ni milioni 336.21 kati ya fedha hizo sh milioni 37.82 ni malipo ya mafundi, sh milioni 298.3 kwa ajili ya manunuzi ya vifaa na sh milioni 3.6 ambazo ni mchango wa jamii.
Getrudi alisema ujenzi wa kituo hicho umefanyika kwa kutumia Force Akaunti kwa kusimamiwa na kamati tatu ambazo ni ya ujenzi, manunuzi na mapokezi na unatarajiwa kukamilika Septemba 30, mwaka huu.
“Pamoja na changamoto kubwa mbili ikiwemo ya kutopatikana kwa maji kwa ajili ya ujenzi pamoja na uwepo wa mwamba mgumu, bado mradi huo unatazamiwa kukamilika ndani ya muda wake Septemba 30, mwaka huu,” alisema.
Vile vile Ujenzi wa Kituo cha Afya cha Chipogoro chenye jengo la waginjwa wan je, vyoo na mfumo wa majisafi na majitaka ulioanza Mei 4, mwaka huu unatazamiwa kugharimu sh milioni 200.
Akisoma taarifa ya ujenzi wa kituo hicho ambacho kinajengwa kwa ajili ya watu ambao walihamishwa kutoka mabondeni kutokana na mafuriko mwaka jana, Mganga Mfawidhi wa Kituo hicho, Dominick Laurian alisema ujenzi huo ambao umekamilika kwa asilimia 95 unatazamiwa kukamilika Septemba 15, mwaka huu.
Kituo hicho ambacho hadi Agosti 30, mwaka huu kimegharimu sh milioni 142.8 pamoja na sh milioni 2.5 za mchango wa kijamii na kufanya jumla y ash milioni 145.3, kimejengwa kwa mfumo wa force akaunti na kusimamiwa na kamati za ujenzi, manunuzi na mapokezi.
Akizungumza Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Jabir Shekimweri alisema, Kituo cha Mtera kiujumla kilianza kufanya kazi tangu mwaka jana, lakini kutokana na mahitaji kuwa makubwa kimeongezewa majengo na hivyo yatakamilika Septemba 30, mwaka huu.
Alisema kituo hicho ni muhimu kwani kitasaidia watu 6,000 wa kata hiyo pamoja na kata jirani watakuwa 12,000 na wananchi wanaosafiri katika barabara hiyo kama watapata ajali au matatizo mengine kutokana na kutokuwa na hospitali kubwa katika barabara hiyo.
Akitoa majumuisho, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Mahenge, kwanza aliwapongeza viongozi wa wilaya pamoja na kamati zilizosimamia vituo hivyo vyote viwili kwani kazi zimeenda vizuri na wananchi watapata huduma bora.
Aliziagiza taasisi mbili muhimu ya maji na umeme kuhakikisha wanakaa pamoja na kuhakikisha huduma hizo zinafika katika kituo cha afya cha Mtera na Chipogoro kabla ya vituo hivyo havijaanza kutoka huduma kikamilifu zikiwemo za operesheni na uzalishaji.
Dkt. Mahenge alimpongeza Rais Magufuli kwa kusema na kutekeleza kwa vitendo kauli yake ya kubadilisha majengo ya makandarasi na kukifanya kituo cha afya na kutoa fedha ili kuongeza miundombinu.
Alisema Rais Magufuli ametoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa vituo na hospitali jumla 32 katika mkoa wa Dodoma vikiwemo vituo vya afya 26 ambavyo vimegharimu takribani sh bilioni 13 na hospitali sita ambazo zimegharibu takribani sh bilioni tisa.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.