Serikali imeunda timu ya watu 12, ambayo itafanya utafiti wa zao la zabibu kama linaleta hasara au faida kwa mkulima na serikali.
Timu hiyo itafanya kazi ndani ya siku 10 pia imeagizwa kujua magonjwa yanayoathiri zao hilo. Kauli hiyo ilitolewa Februari 11, 2020 na Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, alipokuwa akizungumza na wadau wa zao hilo jijini hapa.
Alisema zao hilo ambalo linalimwa mkoani Dodoma linakua kwa kudra za Mwenyezi Mungu, ndio maana ameamua kuunda timu hiyo ambayo itawasilisha ripoti wizarani.
Bashe alisema kuwa zao hilo ndio uti wa mgongo wa wakazi wa Dodoma hivyo kuna haja ya kuweka mpango mkakati kwa ajili ya kuinua zao hilo.
"Kamati ya watu 12 itakayoongozwa na Mwenyekiti Gungu Mibavu, kutoka Ofisi ya DPP, Sera na Mipango ambapo wote watafanya utafiti kwa muda wa wiki moja na kuwasilisha ripoti itakayoletwa na kamati hii itatusaidia kujua wakulima wa zabibu wako wangapi? Changamoto za wakulima, wazalishaji na wasindikaji, hivyo itatusaidia katika mikakati yetu," alisema Bashe.
Alisema mkakati mwingine wa serikali ni kufufua mabwawa yote yaliyotengenezwa kwa ajili ya umwagiliaji wa zabibu katika wilaya tatu zinazolima zao hilo ambazo ni Bahi, Chamwino na Dodoma.
Bashe aliwataka wadau wa kilimo hicho kuunda vyama vya ushirika ili kupata fursa kwenye taasisi za fedha.
Naye Mkurugenzi wa Doniya Estate, ambaye ni msindikaji wa zao la zabibu, Catherine Mwambe, alisema kuwa suala la kodi limekuwa kikwazo kikubwa kwa wazalishaji wa mvinyo.
"Kwa siku moja zinakuja taasisi zaidi ya tano kila moja inakuja kuchukua kodi, hata faida hatupati, maana hela yote inaishia kwenye hizo kodi," alisema Mwambe.
Alisema, gharama za uzalishaji ziko juu na soko la zabibu nchini bado na kuiomba serikali kuingilia kati na kuweka mazingira rafiki ya biashara ya zao hilo.
Chanzo: www.kilimo.go.tz
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.