Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imewashukuru wadau wa maendeleo katika sekta ya afya wanaochangia Mfuko wa Afya wa pamoja kwa kuchangia pesa kiasi cha shilingi bilioni 127 kwa ajili ya kutoa na kuboresha huduma za afya.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu alipofanya ziara ya pamoja na wadau hao katika Kituo cha Afya cha Hombolo Jijini Dodoma kukagua ujenzi wa majengo matano ambayo ni nyumba ya mganga, Maabala, Chumba cha kuhifadhia maiti, Wodi ya kinamama pamoja na Chumba cha Upasuaji.
“Wadau hawa wametupatia shilingi Bilioni 127 kwaajili ya kuboresha huduma za afya, kati ya hizo, bilioni 104 tunazileta kwenye Halmashauri za wilaya pamoja na Sekretarieti za Mikoa ili kuendesha huduma za afya, kwa hiyo hela nyingi zinakuja huku chini kwenye zahanati, kwenye vituo vya afya, kwenye hospitali za wilaya na kule juu tutaweka hela ndogo”
Waziri Ummy amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya Afya Duniani wataendelea kuhakikisha sekta hiyo inapata mafanikio kwa kuboresha huduma za Afya Nchi nzima.
Nae Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Godwin Kunambi ameishukuru Wizara ya Afya pamoja na wadau kwa fedha hizo kwani kwa kiasi kikubwa zimekua zikisaidia kuboresha huduma za Afya hasa katika ngazi ya Zahanati na Vituo vya Afya.
“Jiji la Dodoma tumepokea shilingi milioni 500, na tukazitumia vizuri sana, kwa sababu tulipaswa kujenga majengo matano ambayo yote yamekamilika, lakini sisi hatukuwa nyuma tukasema licha ya kupokea fedha hizi tukaongeza wenyewe milioni 193 kupitia mapato ya ndani, ambapo katika fedha hizo tumetumia milioni 63 kwa ajili ya kujenga Wodi ya watoto, kwa hiyo leo hii zahanati ya Hombolo ina Wodi ya kinamama na Watoto.” alisema Kunambi.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu (kulia) akiteta jambo na Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Godwin Kunambi alipotembelea Kituo cha Afya cha Hombolo kukagua ujenzi wa miundombinu ya majengo ya kituo hicho.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.