Serikali imewataka Watanzania kuwa watulivu kuhusu mlipuko wa ugonjwa wa homa ya corona uliotokea China, na kueleza kuwa hadi sasa hakukna Mtanzania aliyeathiriwa na maradhi hayo.
Hadi sasa ugonjwa huo ambao ulianzika katika Jiji la Wuhan nchini China umeshaua watu zaidi ya watu 80 na zaidi ya 2,000 wakiwa wameambukizwa.
Tangu kugundulika kwa ugonjwa huo, mamlaka ya China imesitisha safari za ndege kwa raia wake wanaotoa na kuingia nchini humo.
Akitoa ufafanuzi kuhusu Watanzania waishio nchini China, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi, aliwataka wawe watulivu, makini na kupenda kuwa na subira ya kupata maelezo au maelekezo na ufafanuzi rasmi wa serikali.
“Watanzania tunaomba muwe na subira ya kupata maelezo au maelekezo na ufafanuzi rasmi wa serikali pale kunakotokea jambo badala ya kukimbilia kwenye mitandao na uvumi ili kuondoa kueneza hali ya taharuki kwa wananchi bila ya kuwa na uhakika,” alisema Prof. Kabudi.
Alisema Tanzania ina wanafunzi takribani 4,000 na kwamba katika mji wa Wuhan wapo 400.
Alisema kwa mujibu wa taarifa ya Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki, ameihakikishia serikali kuwa mpaka sasa hakuna Mtanzania yoyote aliyeathiriwa ama kukumbwa na maradhi hayo.
Alisema Tanzania inaendelea kufuatilia kwa ukaribu kujua maendeleo na hali za Watanzania wanaoishi jimboni Wuhan na China kwa ujumla.
Prof. Kabudi aliwataka Watanzania kuwa makini na suala la kutoa taarifa zisizo rasmi au za uvumi kwa sababu kwa kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.
WATALII 500 WAKWAMA KUJA
Wakati huohuo, mlipuko wa ugonjwa huo umesababisha kusitishwa kwa safari ya watalii zaidi ya 500 waliotarajiwa kuja nchini katika kipindi cha Februari na Machi mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Jaji mstaafu, Thomas Mihayo, alisema watalii hao walitarajiwa kuingia nchini Februari 24 na Machi 2 mwaka huu na ndege za Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL).
“Napenda kuchukua fursa hii kwa masikitiko makubwa kuwajulisha safari za ndege maalumu za ATCL za kuleta wageni, zilizokuwa zimepangwa kufanyika Februari na Machi, zimeahirishwa baada ya serikali ya China kuzuia wananchi wake kusafiri nje ya nchi hiyo, kutokana na mlipuko wa ugonjwa unaosababishwa na virusi vya corona,” alisema Jaji Mihayo.
Kwa mujibu wa taarifa ya TTB iliyotolewa Desemba mwaka jana, Tanzania ilikuwa inatarajia kupokea watalii zaidi ya 500 kwa awamu mbili kutoka China katika kipindi cha Februari 24 na Machi 2 mwaka huu.
Ndege ya ATCL aina ya Boeing 787-8 Dreamliner ndiyo ilitarajia kwenda kuwachukua watalii hao na kuwaleta nchini kwa ajili ya kufanya utalii katika vipindi hivyo viwili.
Chanzo: www.ippmedia.com
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.