WATENDAJI wa Kata katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma wametakiwa kujipanga kuwahudumia wananchi kwa viwango vya juu katika maeneo wanayoyasimia ili kuleta tija katika utumishi wao na hadhi ya makao makuu ya nchi.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru alipokuwa akiongea na watendaji wa Kata wa Jiji hilo jumamosi katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo.
Mafuru alisema “leo nimeona tukae na kutengeneza pamoja dira ya Jiji letu. Mimi napenda tukae pamoja tukubaliane jinsi ya kufanya kazi kwa viwango vya juu kama timu ya ushindi ili wote tukimbie pamoja. Hapa ni makao makuu ya nchi, hivyo, lazima tujipange kutoa huduma bora na kwa kasi na uwezo huo mnao. Kikubwa ninachotegemea kutoka kwenu ni uwajibikaji wenye matokeo chanya. Wapo watendaji wachache nawajua ni wachapa kazi kwelikweli, lakini humuhumu, kuna wengine miyeyusho kwelikweli, hawafanyi kazi zinazotoa matokeo chanya. Wanaishi wanaelea kisanii sanii tu. Mimi natamani wote muwe wachapa kazi”.
Mkurugenzi huyo aliwataka watendaji hao kuwasimamia watendaji wa mitaa na wataalam wote walio katika Kata kutekeleza majukumu yao. “Ninyi ni wasimamizi wa majukumu makubwa sana katika Kata, ukisikia Mkurugenzi, ni watendaji wa Kata. Majukumu yote yapo kwenye Kata, huku makao makuu ni masuala ya kiutawala tu. Nikisema nijifungie tu na wakuu wa Idara tunatengeneza mipango yetu ya utekelezaji, tutakwama tu kwa sababu wakimbizaji wakubwa ambao ni watendaji watakuwa hawajui dira tunayokwenda nayo, ndiyo lengo hasa kukutana” alisema Mkurugenzi Mafuru.
Aliwataka kuhakikisha ofisi za serikali zinafunguliwa kuanzia saa 1:30 asubuhi na kuendelea kuwa wazi hadi saa 9:30 alasiri. “Kwanza muda wa kufungua ofisi ya serikali na muda wa kufunga ofisi ya serikali lazima uzingatiwe. Ujumbe huu uwafikie watendaji wa mitaa wote. Ofisi za umma zipo kwa ajili ya kutoa huduma na kutatua kero za wananchi, lazima ziwe wazi wakati wote na wananchi wapate huduma wanayostahili” alisisitiza Mafuru.
Aidha, aliwataka watendaji wote kuwa na rejista mbili katika ofisi zao, moja ya kuorodhesha migogoro ya ardhi na utatuzi wake, ya pili ya kuorodhesha malalamiko ya kawaida ya huduma za kijamii na hatua za utatuzi wake. Rejista hizo ziwe pia na namba za simu kumrahisishia Mkurugenzi kufuatilia atakapohitaji kufanya hivyo, aliongeza.
Pia aliwataka watendaji hao kuwa na ufahamu mkubwa wa miradi yote ya maendeleo inayotekelezwa katika kata zao na kuwa tayari kuitolea taarifa. “Kuna vitu naona kama hamvimiliki, japo vipo katika kata zenu, mnatakiwa kufahamu shule zinazojengwa, vituo vya afya vinavyojengwa na miradi mingine ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yenu muifahamu kwa kina na kuitolea taarifa ya utekelezaji” aliongeza.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Idara ya Utumishi na Utawala, Innocent Kessy aliwataka Watendaji Kata kusimamia uwajibikaji wa wataalam walio katika kata. “Watendaji lazima mfanye vikao vya kamati za maendeleo ya Kata ambazo wataalam wote katika Kata watawasilisha taarifa za utekelezaji majukumu yao kwa Afisa Mtendaji Kata ili wajumbe wazipitie na wasaidie kuwabana wale wataalam wasiotekeleza majukumu yao” alisema Kessy. Kata zinachangamoto ya usafi, wakati maafisa afya wapo, lazima wasimamiwe vizuri ili watekeleze majukumu yao, aliongeza.
Nae Mhasibu, CPA Rahab Philip aliwataka watendaji Kata hao kuongeza juhudi katika ukusanyaji mapato ya Halmashauri. “Tumeona changamoto nyingi zinazotajwa zinahitaji fedha, kwa habari ya fedha Mkurugenzi hana Kata yake mwenyewe, hata ilipo ofisi ya Mkurugenzi kuna Mtendaji wa Kata. Tunatarajia changamoto zilizoongelewa hapa zitatuliwe kwa kukusanya fedha kutoka kwenye Kata” alisisitiza CPA Philip.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Kata ya Zuzu, Mabruki Seif alimshukuru Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji kwa kuitisha kikao cha watendaji wote na kutoa dira ya Halmashauri katika maendeleo. “Mkurugenzi tunakushukuru sana kwa jinsi ofisi yako inavyoendelea kutoa ushirikiano kwa watendaji kata. Umetupatia meza na viti vipya kwa ajili ya ofisi za Kata. Vifaa hivyo vitaongeza ari ya utendaji kazi kwetu, asante sana” alisema Seif.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.