Na. Asteria Frank, DODOMA
Shirika la Kutetea Haki za Abiria (SHIKUHA) latakiwa kuwapa elimu ya kutosha abiria kwa lengo la kutatua changamoto za usalama barabarani na kufanya abiria wajuwe haki na wajibu wao.
Kauli hiyo imetolewa na Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma, Prof. Davis Mwamfupe, katika mkutano uliofanyika ukumbi wa Rafiki Hoteli Dodoma alipomuwakilisha Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini.
Prof. Mwamfupe alisema kuwa elimu itolewe wakati safari inapoanza ili abiria akipata sehemu ya kujitetea wanakuwa na amani na dereva akienda tofauti na sheria za barabarani waweze kutoa taarifa kuhusu tukio hilo kwa watu sahihi. “Rai yangu kubwa kama kuna kitu ambacho ningewahasa nyie kama shirika kulifanya hili basi ni kuwa na mpango mkakati na huo mpango utaonesha dira yenu kama mlivyosema kwenye risala na lakini mnataka kufikia wapi mwaka huu na je, tunapimaje viongozi maana nyie ni viongozi wa kitaifa kwa kutunza na kusaidia abiria” alisema Prof. Mwamfupe.
Mwenyekiti wa Taifa SHIKUHA, Solomon Nkiggi, alisema kuwa katika kipindi kifupi cha uwepo wa SHIKUHA imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuongeza uelewa wa abiria kuhusu haki na wajibu wao kwa kuwaelimisha abiria kupitia semina, mikutano na matangazo ya vyombo vya habari kwa baadhi ya mikoa. “Changamoto ni nyingi zinazowakabili abiria wetu ikiwemo kupanda kwa nauli isivyo rasmi, ukosefu wa huduma bora kwa baadhi ya maeneo pamoja na ukiukwaji wa haki za msingi za abiria. SHIKUHA imejipambanua kama daraja kati la abiria na watoa huduma za usafiri na serikali kwa lengo la kushughulikia changamoto hizi” alisema Nkiggi.
Kwa upande wake, Muhasisi wa Utetezi wa Abiria Tanzania, Hassan Mchangama, alisema kuwa SHEKUHA inatetea abiria wa nchi kavu na baharini na wamesimamia maeneo yote. Pia watawaelimisha abiria kujua haki zao mbalimbali kwa mujibu wa sheria za nchi ikiwemo za Latra, Usalama barabarani na kimataifa ikiwemo haki ya kupata fidia mtu anapopata ajali.
“Kwenye eneo la ajali kumekuwa na changamoto kubwa sana maana abiria wengi hawajui namna ya kufuatilia haki zao au baadhi ya sheria zimekuwa na changamoto. Matokeo yake abiria wengi nchini Tanzania wanafariki katika ajali, hawalipwi fidia na wanapata majeraha na hawapatiwi matibabu na wengine wanapoteza mali. Tunajua haki mbalimbali zimeimarishwa kutokana na sheria ikiwemo haki ya kusafiri salama” alisema Mchanjama.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.