MKUU wa Mkoa wa Dodoma amewataka Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na Makatibu Tawala Wasaidizi wa Idara mbalimbali za Ofisi ya Mkoa wa Dodoma kushirikiana na kutoa taarifa sahihi za utekelezaji wa maamuzi mbalimbali yanayokubaliwa katika vikao mbalimbali vya Utekelezaji ili kufanikisha utekeleza kikamilifu wa Miradi ya Boost ili kurahisisha utendaji kazi na kukamilisha Miradi hiyo kwa wakati.
Senyamule ameyasema hayo katika kikao kazi cha kujadili Utekelezaji wa Bajeti ya 2022/2023 na Utekelezaji wa Mpango kazi wa Mwaka wa Fedha 2023/2024 kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Jengo la Mkapa kufuatia kutokamilika kwa miradi kwa wakati kama ilivyoelekezwa.
Aidha, Senyamule amewataka Viongozi hao wa ngazi ya Wilaya kuendelea kutunza Mazingira kwa kuanza maandalizi ya kupanda miti na kutenga maeneo ya kuoteshea vitalu vya Miche ya miti kwaajili ya kupanda wakati wa Msimu wa Mvua unapokaribia ili kuwe na miche ya kutosha kwa kila Halmashauri kupanda miti milioni moja na laki tano kwa Mwaka kwa mujibu wa maelekezo ya Serikali.
"Katika kuendelea kukijanisha Mkoa wetu na kutunza Mazingira yetu tuanze mapema maandalizi ya kuandaa vitalu vya miche na kila wilaya iwe na Miche ya kutosha isiyopungua milioni moja na laki tano kama agizo lilivyotolewa na Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hapa nisisitize kuwa katika kila wilaya nitakayofanya ziara kuanzia mwezi huu nitakagua vitalu hivyo vilevile hakikisheni mnatenga maeneo kwa ajili ya kunufaika na biashara ya hewa Ukaa na kila Wilaya angalau iwe na maeneo matatu kama tulivyokubaliana hapo awali". Amesisitiza Senyamule
Kwa upande wake Afisa Elimu wa Mkoa wa Dodoma Bw. Gift Kyando ametoa rai wilaya zilizokamilisha ujenzi wa Shule na madarasa kupitia fedha za mradi Boost kuanza usajili wa Shule hizo mapema ili zianze kupokea wanafunzi ifikapo Mwezi Januari 2024.
"Kwa Halmashauri ambazo zimekamilisha ujenzi wa Miradi hii zinatakiwa kuanza usajili ili mwakani tuanze kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza na kuwahamishia wanafunzi wa kidato cha pili na tatu kwa wale wanaotoka maeneo ya mbali na Shule wanaposoma kwa sasa hii itawarahisishia masomo yao".
Katika kuendelea kuboresha na kuweka miundombinu rafiki kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu Bw. Kyando amewaomba wasanifu ramani za Majengo ya Miradi hiyo kuandaa ramani rafiki kwa wanafunzi Wenye Ulemavu wa viungo na zitakazotumia gharama ndogo huku zikiwa na Ubora unaohitajika.
Kikao hiki cha kujadili utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2022/23 na Utekelezaji wa Mpango kazi wa mwaka 2023/24 pia kimejadili miradi ya elimu kupitia fedha za boost na SEQUIP. Pia, wajumbe walipata fursa ya kutambulishwa katika program endelevu ya usafi wa mazingira na upatikanaji wa maji Vijijini na Mfumo wa Dharura wa Rufaa wa usafirishaji wa wajawazito na watoto wachanga.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.