Na. Dennis Gondwe, DODOMA
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma inajenga shule ya msingi ya mtaala wa kiingereza ili kutoa elimu bora itakayowasaidia wanafunzi kupata maarifa na umahiri katika masomo ili wawe wataalam wa nyanja mtambuka nchini na kulisaidia taifa kufikia mapinduzi ya kiuchumi.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Idara ya Elimu Msingi Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Prisca Myalla alipokuwa akisoma taarifa ya ujenzi wa shule ya msingi ya mtaala wa kiingereza kwa kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Sahili Geraruma katika eneo inapojengwa shule hiyo Kata ya Dodoma Makulu jijini hapa.
Myalla alisema kuwa lengo la mradi huo ni kutoa elimu bora itakayowasaidia wanafunzi kupata maarifa na ujuzi utakaowawezesha kuwa wanafunzi mahiri katika masomo. “Elimu hiyo itawawezesha kuwa wataalam katika nyanja mbalimbali ndani na nje ya nchi na kusaidia taifa kufikia mapinduzi ya kiuchumi yatakayoiwezesha Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati. Lengo lingine ni kuwezesha wanafunzi na walimu kuwa na mahali pazuri pakujifunzia na kufundishia. Pamoja na kuongeza uandikishaji wa wanafunzi wa awali kutoka 13,056 kwa mwaka 2022 hadi 17,556 kwa mwaka 2025. Pia kuongeza uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la kwanza kutoka 19,494 kwa mwaka 2022 hadi 23,994 kwa mwaka 2025” alisema Myalla.
Akiongelea hali ya utekelezaji wa mradi huo, alisema kuwa mradi ulianza tarehe 20.05.2022 kwa halmashauri kupata eneo lililopimwa katika kiwanja namba 20 na 21 Kitalu C Mapinduzi East chenye ukubwa wa Hekta 3.71 sawa na Ekari 9.17 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya shule na viwanja vya michezo. “Hali ya utekelezaji kwa upande wa vyumba vinane vya madarasa viko hatua ya renta, matundu 32 ya vyoo vya wavulana na wasichana hatua ya kupaua na jengo la utawala hatua ya skimming. Hadi sasa jumla ya shilingi 298,243,133.10 zimeshatumika ikiwa ni pamoja na ununuzi wa vifaa vya ujenzi, malipo ya mafundi, gharama za uingizaji umeme na maji eneo la mradi, gharama za upimaji wa nondo, tofali, kokoto na mchanga. Halmashauri inatarajia kukamilisha ujenzi wa mradi huu ifikapo mwezi Oktoba, 2022” alisema Myalla.
Halmashauri ya Jiji la Dodoma ilipokea jumla ya shilingi 750,000,000 tarehe 30 Machi, 2022 kutoka Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kwa ajili ya ujenzi wa shule ya mtaala wa kiingereza.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.