Na. Theresia Nkwanga, DODOMA
KAMATI ya Fedha na Utawala ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma imepongeza usimamizi wa mradi wa ujenzi wa madarasa mawili na mabweni mawili katika shule ya sekondari ya Bihawana kwa gharama ya shilingi 240,000,000.
Pongezi hizo zilitolewa na kiongozi wa kundi namba moja, Diwani Gombo Dotto alipoongoza kundi hilo kutembelea na kukagua utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa madarasa mawili na mabweni mawili ya shule ya sekondari Bihawana iliyopo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Diwani Dotto alisema “mradi tumeukagua ni mzuri unaakisi fedha zilizotumika. Taarifa ya mradi tumeisoma imeandaliwa vizuri, niwapongeze kwa usimamizi mzuri wa mradi huu. Ni matumaini yangu mtaukamilisha haraka sababu vifaa vyote mnavyo pia nimpongeze Afisa Elimu Sekondari, Upendo Rweyemamu kwa utendaji wake mzuri wa kazi na usimamizi”.
Aidha, alishauri kutumia ‘Marine board’ badala ya mbao ili kupunguza gharama za ujenzi. ‘Marine board’ huweza kutumika zaidi ya mara moja tofauti na mbao ambazo zikimaliza kazi haziwezi kutumika tena kutokana na kupinda, aliongeza.
“......kama majengo ni mengi ni vema mfikirie kutumia “marine board” ambazo gharama yake ni nafuu ukilinganisha na mbao, pia mbao zinatumika nyingi sana kwenye ujenzi tofauti na ‘marine’ na zikishatumika ni ngumu kuzitunza kwaajili ya matumizi ya badae mwisho wa siku zinakosa pakwenda zinaishia kutupwa au kutumika kama kuni”.
Nae Mkuu wa shule ya sekondari Bihawana, Liberatus Ntilema alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutatua changamoto za msongamano wa wanafunzi katika madarasa na mabweni. Vilevile, aliushukuru uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa maelekezo makini na ushauri wa mara kwa mara katika ujenzi unaoendelea. “Mradi huu unagharimu kiasi cha shilingi milioni 240,000,000, fedha za Mpango wa Uboreshaji wa Elimu ya Sekondari (SEQUIP)” alisema Ntilema.
Akiongelea changamoto zinazoukabili ujenzi huo, Ntilema alizitaja kuwa ni kuchelewa kwa kuwekewa vifungu vya malipo ya mradi wa SEQUIP hali iliyosababisha fedha za mradi kuvuka mwaka wa fedha 2021/22 bila kutumika. Nyingine ni ongezeko la bei kwa vifaa vya ujenzi na gharama kubwa za usafiri kutoka mahali vifaa vilipo hadi shuleni. Kukosekana kwa fedha ya ufatiliaji wa maswala yote ya ujenzi na uchelewaji wa kufunguka mfumo wa FFARS kwa mwaka mpya wa fedha 2022/2023 kumechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza kasi ya ujenzi, aliongeza.
Alimalizia kwa kuelezea changamoto zinazoikabili shule ya sekondari Bihawana kuwa ni shule kutokuwa na walimu wa kutosha kulingana na idadi ya wanafunzi. Nyingine ni shule kutokuwa na jiko la kupikia na shule kutokuwa na bwalo kubwa linaloendana na idadi ya wanafunzi na shule kukosa ukumbi wa mikutano.
Shule ya sekondari Bihawana ina jumla ya wanafunzi 838 ambao wote ni wavulana wa kidato cha Tano na Sita katika tahasusi za CBA, CBG, HGL, PCB na PCM kati ya wanafunzi hao 361 (41%) ni wa kidato cha Tano na kidato cha Sita ni 477 (58.9%) ikiwa na jumla walimu 27 kati ya hao wa kiume ni 19 na wa kike ni 8.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.