Halmashauri ya Jiji la Dodoma, imemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa uamuzi wake wa kukarabati mabweni ya shule ya Wasichana ya Msalato Jijini hapa hatua ambayo imeongeza ufaulu wa wanafunzi kutokana na uwepo wa mazingira mazuri ya kusomea.
Hayo yamesemwa na Afisa Elimu ya Sekondari wa Jiji la Dodoma Mwalimu Upendo Rweyemamu alipokua akizungumza na mwandishi wetu ofisini kwake kuhusu kupanda kwa ufaulu wa Jiji la Dodoma katika matokeo ya kidato cha sita mwaka 2020.
Mwalimu Rweyemamu alisema kuwa shule ya wasichana ya Msalato imepanda kutoka nafasi ya 81 mwaka 2019 hadi kufikia nafasi ya 15 kitaifa katika matokeo ya kidato cha sita mwaka 2020.
“Kitendo cha Mhe. Rais, Dkt. John Pombe Magufuli cha kukarabati shule kongwe nchini ikiwemo shule yetu ya wasichana Msalato, ndicho hasa kilichochangia matokeo haya, pamoja na juhudi za walimu, lakini mazingira ya ufundishaji na kufundishia yamebadilika sana jambo linalowapa wanafunzi wetu hamasa ya kusoma” Alisema Mwalimu Rweyemamu.
Aidha alisema kuwa Serikali ilitoa kiasi cha shilingi milioni 937.5 kwa shule ya wasichana Msalato kwa ajili ya kukarabati mabweni nane, ambayo tayari yamekwisha karabatiwa na wanafunzi wanalala katika mazingira safi na salama tofauti na ilivyokuwa awali.
“Ukiitembelea Msalato sasa ni tofauti kabisa na ilivyokua mwanzo, inapendeza sana lakini sio kuongeza ufaulu kwa wanafunzi tu bali hata walimu hawapati kazi kubwa kufundisha kwa sababu yule wanayemfundisha tayari akili yake imekaa kwenye utayari wa kupokea anachofundishwa kutokana na mazingira mazuri yaliyowekwa na Rais wetu” Aliongeza Mwalimu Rweyemamu.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.