KATIBU Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhandisi Joseph Nyamhanga amesema Serikali imewapangia waalimu wengi zaidi wa shule ya msingi katika shule za vijijini ambako ndiko kwenye upungufu mkubwa wa waalimu.
Akiongea na vyombo vya habari leo kuhusu ajira mpya za waalimu wa shule za Msingi na Sekondari pamoja na mafundi sanifu wa maabara, Mhandisi Nyamhanga amesema kuwa kwa upande wa shule za msingi upangaji wa waalimu umefanyika kwa lengo la kuboresha uwiano wa waalimu kwa wanafunzi.
Mhandisi Nyamhanga amesema kuwa asilimia 60 ya walimu wote walioajiriwa wamepelekwa katika shule za msingi hasa za vijijini ambako ndiko kwenye uhitaji mkubwa wa waalimu nchini.
Ameendelea kufafanua kuwa Serikali imeweka kipaumbele kuajiri waalimu kwa ajili ya shule za sekondari zenye mchepuo wa sayansi na Hisabati, ufundi, kilimo na maarifa, maarifa ya nyumbani, lugha ya kiingereza, kichina na kifaransa.
Amesema kuwa walimu wa masomo mengine wamepangwa kulingana na upungufu uliopo ambapo kipaumbele ni shule ambazo hazina walimu wa masomo husika.
Mhandisi Nyamhanga amesema pia wamezingatia shule zenye mahitaji maalum ambako waalimu 481 wameajiriwa kwa ajili ya shule hizo na kuwa suala la umri wa ajira za Serikali limezingatiwa na waalimu waliopata ajira ni wale waliomaliza chuo mwaka 2014 mpaka 2019.
Aidha, Mhandisi Nyamhanga amesema kuwa waajiriwa wapya wa uwaalimu wa shule za Msingi na Sekondari wanatakiwa kuhakikisha wanaripoti katika vituo walivyopangiwa ndani ya muda wa siku 14, kinyume na hapo watakuwa wamepoteza nafasi zao na zitajazwa na waombaji wengine.
“waajiriwa wapya wanatakiwa kuripoti kazini kuanzia tarehe 1 hadi tarehe 14 Desemba 2020 watakaoshindwa kuripoti nafasi zao zitajazwa na waombaji wengine wenye sifa waliopo kwenye kanzidata ya Ofisi ya Rais –TAMISEMI”, amesisitiza Mhandisi Nyamhanga.
Vile vile amewaagiza wakurugenzi wa Halmashauri ambao walimu hao wamepangiwa kuwapokea na kuwawezesha kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya utumishi wa umma.
Hata hivyo amewaagiza wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha wanatoa taarifa ya kuripoti waajiriwa hao na kuzijaza kwenye mfumo wa kielektroniki baada ya kila mtumishi kupokelewa katika kituo cha kazi.
“Kamilisheni taratibu za ajira haraka ili walimu hawa waingizwe katika mfumo wa malipo ya mshahara (payroll) mapema iwezekanavyo”, ameelekeza Mhandisi Nyamhanga.
Tarehe 7 Septemba, mwaka huu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli alitoa kibali cha ajira mpya za walimu 13,000 wa shule za Msingi na Sekondari pamoja na Mafundi Sanifu wa Maabara za Shule.
Kuona Orodha bofya hapa: TAARIFA YA ORODHA YA MAJINA NA VITUO VYAO
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.