MGOMBEA nafasi ya uongozi katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2019 anatakiwa kuwa hajawahi kupatikana na hatia kwa kosa la utovu wa uaminifu katika kipindi cha miaka mitano kabla ya tarehe ya uchaguzi.
Kauli hiyo ilitolewa na msimamizi wa uchaguzi wa serikali za mitaa katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dickson Kimaro (aliyesimama pichani) alipokuwa akitoa maelezo kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa ngazi ya Mitaa utakaofanyika tarehe 24 Novemba, 2019, kwa viongozi wa vyama vya siasa na Wasimamizi Wasaidizi ngazi ya Kata katika Halmashauri hiyo kwenye kikao kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji leo.
Akiongelea sifa za mgombea katika uchaguzi wa serikali za mitaa, Kimaro alisema “mgombea awe hajawahi kupatikana na hatia kwa kosa la utovu wa uaminifu katika kipindi cha miaka mitano kabla ya tarehe ya uchaguzi. Sifa nyingine awe hana ugonjwa wa akili uliothibitishwa na daktari anayetambulika na serikali au bodi ya utabibu” alisema Kimaro. Sifa nyingine alizitaja kuwa mgombea huyo awe mwanachama wa chama cha siasa na amedhaminiwa na chama hicho.
Msimamizi huyo wa uchaguzi aliongeza kuwa mgombea anatakiwa kuwa na shughuli halali ya kumuwezesha kuishi na akiwa mkazi wa wa eneo la mtaa husika. “Mgombea lazima awe raia wa Tanzania, awe na umri wa miaka 21 au zaidi. Pia awe na uwezo wa kusoma na kuandika Kiswahili au kiingereza” aliongeza msimamizi huyo wa uchaguzi huyo.
Akiongelea uteuzi wa wagombea, alisema kuwa uteuzi huo utafanyika tarehe 05/11/2019 kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni. “Fomu za maombi ya uteuzi wa kugombea nafasi ya uenyekiti wa mtaa pamoja na wajumbe wa kamati ya mtaa zitatolewa na kupokelewa kwenye ofisi za wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi katika kata zote kuanzia tarehe 29/10/2019 hadi tarehe 05/11/2019 saa 1:30 asubuhi hadi saa 10:00 jioni kila siku” alisema Kimaro.
Kuhusu kupiga kura, alisema kuwa uchaguzi wa mwenyekiti wa mtaa na wajumbe wa kamati za mitaa utafanyika kwenye vituo vya kupigia kura vilivyoko kwenye mitaa iliyoko kwenye orodha iliyotangazwa na serikali ya maeneo ya utawala ya halmashauri ya jiji la Dodoma tarehe 24/11/2019. “Siku ya kupiga kura, msimamizi wa kituo anaweza kumtaka mpiga kura aoneshe kitambulisho ili kujiridhisha kama jina lake lipo kwenye orodha ya wapiga kura. Aina ya vitamvulisho hivyo ni kitambulisho cha mpiga kura, kitambulisho cha kazi, hati ya kusafiria, kadi ya benki na kadi ya bima ya afya. Vingine ni kitambulisho cha shule au chuo, kitambulisho cha mifuko ya hifadhi ya jamii na kitambulisho cha taifa” alibainisha msimamizi huyo.
Wakati huohuo, Mkuu wa Kitengo cha Uchaguzi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Hidaya Maeda alisema kuwa kanuni za uchanguzi wa viongozi wa mamlaka za serikali za mitaa ngazi ya vijiji, vitongoji na mitaa za mwaka 2019 zinaelekeza msimamizi wa uchaguzi kutoa maelezo kuhusu uchaguzi wa serikali za Mitaa utakaofanyika tarehe 24 Novemba, 2019. “Vituo vya kupigia kura vipo 383, na tutawapatia orodha hiyo. Idadi ya wapiga kura itapatikana baada ya kuandikisha wapiga kura na tutabandika baada ya daftari kukamilika” alisema Maeda.
Kwa mujibu wa kanuni, kampeni zimepangwa siku saba na kuwataka kutofanya kampeni kabla ya muda kwa kuwa kufanya hivyo ni ukiukwaji wa kanuni.
Aidha, aliwataka wananchi wenye sifa ya kupiga kura kujitokeza kujiandikisha kipindi cha uandikishaji katika ngazi za mitaa wanayoishi,wale wenye sifa za kugombea kutimiza haki yao ya Kikatiba kugombea kupitia vyama vyao na mwisho siku ya kupiga kura wale wote watakaokuwa wamejiandishisha kujitokeza kupiga Kura .
Kikao hicho kilihudhuriwa na vyama vya siasa vya CCM, Chadema, ACT Wazalendo, UMD, Sauti ya Umma, NCCR Mageuzi, CUF na Demokrasia makini.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.