Aliyoyasema Rais Dkt. John Pombe Magufuli
Naipongeza Sekta ya Sheria na Mahakama nchini kwa kupata mafanikio makubwa ikiwemo kupungua kwa muda wa usikilizwaji wa kesi, kuimarisha matumizi ya TEHAMA pamoja na kuanzisha Mahakama zinazotembea.
Matumizi ya TEHAMA yamepunguza utoaji na upokeaji wa rushwa pia yameongeza kasi ya ukusanyaji wa maduhuli kutoka shilingi Bil.1.6 kwa mwaka 2017 hadi shilingi Bil.2.6 mwaka 2019.
Mafanikio ya Mahakama pia yamechangiwa na uamuzi wa Serikali wa kuteua Majaji 11 wa Mahakama ya Rufani, Majaji 39 wa Mahakama Kuu pamoja na kuajiri Mahakimu wapya 396.
Uanzishwaji wa Mahakama ya Mafisadi umeondoa dhana iliyokuwa imejengeka miongoni mwa wananchi kuwa mapambano ya rushwa nchini yamekuwa yakiwalenga wananchi wa chini na kuwaacha vigogo.
Tangu Mahakama hii ianzishwe mwaka 2016 jumla ya Mashauri ya uhujumu uchumi 119 yamesajiliwa na mashauri 89 yamemalizika ambapo faini ya sh.Bil 13.6 na fidia ya Bil. 30.6 zimetolewa.
Nakuhakikishia kuwa tutakupatia fedha za kujenga Mahakama ya Jijini Dodoma, pia kati ya watumishi 268 uliowaomba, tutaajiri watumishi 200 ili wakafanye kazi katika Mahakama mpya zinazojengwa.
Katika magereza yetu kuna jumla ya wafungwa 13,455 na mahabusu 17,632 hii inaonesha kuna ucheleweshwaji wa kesi hivyo wapelelezi hakikisheni mnaharakisha upelelezi kwani mnawanyima watu haki.
Bado kuna changamoto ya migogoro ya ardhi na dhuluma kwa wanawake hasa wajane, sina uhakika kama Mabaraza ya Ardhi yanafanya kazi vizuri pengine yapo chini ya Wizara ya Ardhi lakini lawama zinapotolewa zinarudi kwa Mahakama hivyo migogoro hiyo ifanyiwe kazi.
Serikali imepeleka Muswada wa Sheria ya Usuluhishi ili kufuta Sheria hizo za mwaka 1932, tunaamini sheria mpya itaziwezesha Mahakama zetu kufanya usuluhishi na tutaweza kuendana na mikataba mbalimbali ya kimataifa tuliyosaini.
Aliyoyasema Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma
Siku ya Sheria ni muda mzuri kwa wananchi kukumbushana umuhimu wa Katiba na Sheria katika kuwawezesha Watanzania kuendelea kuishi pamoja katika nchi huru na kutafakari namna ambayo Sheria itatumika kuwezesha kufanikisha ukuaji wa uchumi.
Kauli mbiu ya mwaka huu inawataka watumishi wa umma walio na majukumu ya kutekeleza sheria mbalimbali wajitathimini kama wanatumia sheria na taratibu za mahakama sio kwa lengo la kuweka vikwazo bali kuendeleza biashara na uwekezaji.
Tumesimika vifaa vya mawasiliano kwa njia ya video katika baadhi ya ofisi zetu ambapo hadi sasa mashauri 60 ya Mahakama ya Rufani yamesikilizwa kwa kutumia mfumo huo pamoja na kusikiliza mashahidi waliopo nje ya Tanzania.
Chanzo: IDARA YA HABARI - MAELEZO
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.