Timu ya Dodoma Jiji FC jana imepoteza mchezo wake dhidi ya wenyeji Simba ya Dar es Salaam kwa kufungwa magoli 3 – 1 katika mchezo mkali uliofanyika kuanzia saa 1 usiku katika uwanja wa Benjamin Mkapa.
Simba ndio walikua wa kwanza kupata goli katika dakika za mwanzo za mchezo na baadae Dodoma Jiji kuushika mchezo na kufanikiwa kurejesha goli hilo kupitia kwa mchezaji wake wa kati Cleophace Mkandala mnamo dakika ya 29 ya mchezo goli lililodumu mpaka kipindi cha mapumziko.
Baada ya kurejea katika kipindi cha pili Simba walionekana kurudi mchezoni na kupachika magoli mengine mawili na kufanya mechi hiyo kumalizika kwa Dodoma Jiji kufungwa goli 3 – 1.
Akizungumza baada ya mchezo huo kocha Mkuu wa Dodoma Mbwana Makata alisema kuwa anawapongeza wachezaji wake kwa kupambana na kuonesha mpira mzuri muda wote wa mchezo na kwamba matoke hayo hayawarudishi nyuma katika mapambano yao ya kumaliza ligi katika tano za juu.
Makata alisema kuwa Simba ni timu kubwa na ina wachezaji wenye uzoefu na ligi hivyo anaamini kadri siku zinavyosogea na kikosi chake pia kitaendelea kuimarika na kufanya vizuri Zaidi.
“Matokeo haya hayatuvunji moyo, tuna michezo mingine inakuja kwaiyo tukiruhusu matokeo haya yatufanye wanyonge tutapoteza malengo na tutaishia kufanya vibaya kwenye ligi kwaiyo nimewaambia vijana wangu wamejitahidi na tunasafari ndefu ya kwenda basi kazi iendelee” Aliongeza Makata.
Matokeo hayo yanawafanya Dodoma Jiji kusalia katika nafasi ya sita wakiwa na pointi 38, huku akicheza michezo 28.
Tayari Kikosi cha Dodoma Jiji FC leo kimeanza safari ya kurejea Jijini Dodoma baada ya kupoteza mchezo wake dhidi ya Simba hapo jana katika dimba la Mkapa.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.