HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma yapongezwa kwa kutumia asilimia 75 ya mapato yake ya ndani katika miradi ya maendeleo likiwa ni ongezeko zaidi ya asilimia 15 ya maelekezo ya serikali.
Pongezi hizo zilitolewa na waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Seleman Jafo alipokuwa akitoa salamu zake katika mkutano wa mwaka wa baraza la madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dodoma jana katika ukumbi wa mikutano wa Jiji hilo.
Waziri Jafo alisema “nilikuwa nikipitia miradi yenu, zaidi ya asilimia 75.6, ambapo ninyi mmewekewa malengo kuwa si chini ya asilimia 60 iende kwenye miradi ya maendeleo. Ninyi mmevuka viwango zaidi ya asilimia 75. Maana kukusanya ni jambo lingine na kupeleka katika matumizi sahihi ni jambo jingine pia. Mmekusanya vizuri na mmepeleka kwenye miradi ya maendeleo. Na kilichonifurahisa sana ni mpango wenu wa kubuni miradi ya kimkakati mikubwa ya kusaidia Halmashauri yenu kuongeza mapato. Dodoma tunataka iwe tofauti na hii tofauti naiona. Kwa vile mmeshatenga bajeti safari imeanza. Mimi nitawapigania, Dodoma tunataka Jiji la mfano miradi ya kimkakati itekelezwe” alisema Waziri Jafo.
Waziri huyo aliitaka Halmashauri hiyo kusimamia vizuri utekelezaji wa miradi ya kimkakati ili thamani ya fedha ionekane. “Mjiepushe na wakandarasi makanjanja. Wanaopita maofisini kwenda kudai kazi. Zingatieni sheria ya manunuzi” alisema Waziri Jafo.
“Mstahiki meya niwapongeze kwa kazi kubwa mnayoendelea kuifanya katika Jiji la Dodoma. Jiji la Dodoma katika Mamlaka za Serikali za Mitaa 185 ambazo Mheshimiwa Rais amenipa kuzisimamia, sina mashaka ya aina yoyote, ninaposema kwamba katika Mamlaka za Serikali za Mitaa isiyonisumbua kichwa kabisa ni Jiji la Dodoma, sina mashaka kabisa” alisema kwa kujiamini Waziri Jafo.
Vilevile, alipongeza mipango mizuri inayotekelezwa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma na kujiondoa katika utegemezi wa kiwango kikubwa kwa serikali kuu. “Leo hii Halmashauri nyingine utegemezi ni zaidi ya asilimia 90. Ninyi Halmashauri yenu mpo mbali sana” alisema Waziri Jafo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.