HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imepata mafanikio makubwa katika kipindi cha miaka mitano tangu serikali ya awamu ya tano kuingia madarakani kutokana na umoja wa Baraza la Madiwani na watendaji jambo lililoiwezesha kutoa huduma bora kwa wananchi.
Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Prof. Davis Mwamfupe wakati akihutubia Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo kabla wa kulivunja rasmi tukio lililofanyika katika ukumbi wa mikutano wa chuo cha Mipango Dodoma.
Prof. Mwamfupe alisema kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma imepiga hatua kubwa katika utoaji huduma bora kwa wananchi. Alisema kuwa jukumu kubwa la Halmashauri ni kutoa huduma bora kwa wananchi, kama tulivyosikia taarifa ya mafanikio ya Halmashauri iliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Jiji. “Mafanikio yetu haya makubwa yanatokana na ukweli kuwa tumedumu wamoja kama Baraza la Madiwani. Mafanikio haya ni matokeo ya uongozi bora, amani na uwazi. Shukrani kwa Mheshimiwa Rais, Dkt. John Magufuli kwa kutoa dira kwa taifa na kuhimiza watumishi na wananchi kufanya kazi. Lakini wakati huohuo, serikali hii imejipambanua kutokubembeleza watumishi wazembe. Kwa uzito huohuo, tunamshukuru kwa kutupa Makao Makuu Dodoma, tunamhakikishia kuwa tutaendelea kutekeleza wajibu wetu wakuwahudumia wananchi” alisema Prof. Mwamfupe.
Akiwasilisha taarifa ya mafanikio ya shughuli za Halmashauri kuanzia mwaka 2014/2015 hadi 2019/2020, Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi alisema kuwa Halmashauri imeendelea kupata mafanikio makubwa katika utoaji huduma bora kwa wananchi kupitia idara, vitengo na mamlaka zilizopo. Alisema kuwa katika kipindi cha miaka mitano ya serikali ya awamu ya tano Jiji la Dodoma limefanikiwa kuongeza ukusanyaji mapato kwa asilimia 1,349. “Jiji la Dodoma limeweza kuongeza na kukusanya mapato ya ndani kutoka bajeti ya shilingi 4,554,075,181 kwa mwaka 2015/2016 hadi shilingi 66,010,324,746 kwa mwaka 2019/2020 sawa na ongezeko la asilimia 1,349” alisema Kunambi.
Akiongelea hoja za ukaguzi, alisema kuwa Jiji la Dodoma limeweza kujibu na kupunguza hoja za ukaguzi zilizotolewa na CAG kutoka hoja 161 mwaka wa fedha 2015/2016 hadi hoja 46 mwaka 2018/2019 sawa na asilimia 71. Alisema kuwa kuanzia mwaka 2016/2017 hadi 2018/2019 Halmashauri ya Jiji imeendelea kupata hati safi ya ukaguzi.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa mafanikio ya miaka mitano ya serikali ya awamu ya tano yanatokana na juhudi za pamoja kati ya serikali kuu, Halmashauri ya Jiji la Dodoma, wananchi pamoja na wadau waliohusika katika kuchangia michango mbalimbali ya maendeleo.
Katika salamu za Mkuu wa Wilaya ya Dodoma mjini, Patrobas Katambi alilipongeza Baraza la Madiwani chini ya uongozi wa Mstahiki Meya kwa kazi nzuri. “Mkurugenzi wa Jiji amefanya kazi kubwa inayoonekana kwa ushirikiano na menejimenti yake na taasisi zote jijini hapa” alisema Katambi. Aidha, alieleza matarajio yake kuwa Halmashauri itaendelea kutatua changamoto zitakazojitokeza katika kuwatumikia wananchi.
Kwa upande wake Ephrahim Matonya mwananchi aliyekuwa akifuatilia mkutano wa Baraza la Madiwani moja kwa moja kupitia njia ya mtandao alisema kuwa Jiji la Dodoma linaonesha mafanikio yajayo. Kwa miaka hii michache Dodoma kuna maendeleo makubwa aliongeza. “Zamani watu walikuwa wakiondoka kutoka Dodoma kwenda mikoa mingine, sikuhizi tunaona watu wengi wanakimbilia Dodoma” alisema Matonya.
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dodoma limevunjwa rasmi na majukumu yake kukasimiwa kwa timu ya wataalam ya Halmashauri hiyo kwa kipindi chote hadi baraza lijalo litakapoapishwa.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.