SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, ameweka wazi kuhusu tozo ya miamala katika simu kwa kusema kuwa Bunge ndio liliamua na kupitisha na wale ambao wanapinga wanatakiwa kutoa mawazo mbadala ya nini kifanyike wakati akisisitiza lengo ni ifikapo mwaka 2025 Tanzania liwe Taifa tofauti katika suala la maendeleo.
Msimamo huo aliutoa katika kikao kazi cha viongozi wa Mkoa na wilaya zote za Dodoma kilichoandaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na kufanyika katika ukumbi wa Kitivo cha Teknolojia ya Habari na Elimu Angavu katika Chuo kikuu cha Dodoma.
Akifafanua kuhusu adhima ya wabunge kuona baadhi ya mambo ya kimaendeleo yanasonga mbele alisema “Sisi pale Bungeni tumekaa na kufikiri sana kama watumishi wenu namna gani tunaweza kumaliza baadhi ya mambo ili tusonge mbele, tunataka ifikapo mwaka 2025 kisiwepo kijiji Tanzania nzima ambacho hakina huduma ya Umeme, ni lengo kubwa. Sasa tuna lengo la kuhakikisha kwamba kumtua ndoo mama kichwani ni jambo ‘reality’ (halisi) kupeleka maji vijiji vyote, tuna uhaba mkubwa sana wa madarasa ya shule za msingi na sekondari ni uhaba mkubwa kweli kweli, tunataka jambo hilo liwe historia. Tuna uhaba mkubwa sana wa madawati… hatutaki kuona mtoto anakaa chini, tunajaribu kuona kwamba kila kijiji kufikia mwaka 2025 kina Zahanati, haya ni malengo makubwa” alisema Spika Ndugai kwa uchungu.
Akiongelea ufikiaji wa malengo hayo makubwa ifikapo mwaka 2025, alisema kuwa utekelezaji wa sheria hiyo ni muhimu. “Tunayafikiaje malengo haya… ndio maana sisi wabunge tukaamua kwamba tunakwenda kwenye miamala, hasa ukinuna sawa ukifanyaje sawa, tunakwenda kwenye miamala. Tutatoza kakitu fulani (fedha kidogo) kwenye miamala, fedha inayopatikana sio kodi ya kawaida, inakwenda katika mfuko maalumu na fedha ile itarudishiwa wananchi wenyewe kupitia hayo maji, umeme, barabara za vijijini zote, madaraja, afya na kadharika, kupitia hii tozo ndogo ndogo ya kwenye miamala” alisisitiza Spika huyo.
Akiongelea sheria hiyo ya miamala, alisema kuwa, imetungwa na wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi. “Tumepitisha sisi, tukatunga sheria sisi, tunataka kuliona hilo, hakuna atakaekuja kutujengea nchi hii (amesema Profesa hapa). Unaepinga hilo sawa, tupe mbadala tunawezaje kuyafanya haya ifikapo 2025? Tutapata wapi fedha?... inawezekana kiwango ni kikubwa inatakiwa iwe kidogo kidogo hilo lina mjadala wake. Lakini lazima tufanye, kama tunavyofanya kwenye mambo mengi… mtu wetu wa kijijini awe kwenye darasa zuri lenye ‘tiles’ kama mtu wa mjini, apate huduma ya afya kama mtu mwingine yeyote. Kwa hiyo maamuzi haya tumeyafanya kwa nia njema kabisa kwamba mwaka 2025 tuwe ni taifa la Tanzania ambalo ni tofauti Afrika nzima” alisema Spika Ndugai.
Kikao kazi hicho kilihudhuriwa na wajumbe takribani 600 ikijumuisha Spika wa Bunge, Mkuu wa Mkoa, Katibu Tawala wa Mkoa, Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (Mkoa na Wilaya), Kamati ya Usalama (Mkoa na Wilaya), Wabunge, wakuu wa Wilaya, Mstahiki Meya wa Jiji, Wenyeviti wa Halmashauri, Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa. Wengine ni Wajumbe wa Timu ya Menejimenti ya Mkoa, Makatibu Tawala wa Wilaya, Wakuu wa Taasisi mbalimbali, Madiwani wa Halmashauri zote, Wajumbe wa Timu za Menejimenti wa Halmashauri zote na Waandishi wa Habari.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.