MKURUGENZI wa Jiji la Dodoma Godwin Kunambi ameongea na waandishi wa Habari mapema leo katika ukumbi wa Jiji la Dodoma na kuutaarifu umma wa Watanzania juu ya ufunguzi wa miradi ya kimkakati ya Jiji la Dodoma ambayo imekamilika na inatarajiwa kuanza kutumika mwezi huu wa Aprili.
Maradi hiyo iliyoanza kujengwa na kampuni ya Mohamed Builders miezi 15 iliyopita sasa imekamilika na miradi yote yaani kituo kikuu cha mabasi, Soko kuu la Ndugai, kituo cha kupumzikia cha Chinangali na kituo cha kuegesha malori imeshakabidhiwa kwa Halmashauri ili ianze kufanya kazi kwa kuwahudumia Wananchi.
“Baada ya kukamilisha ujenzi huu mkandarasi amekabidhi miradi kwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma na Halmashauri inatangaza fursa kwa Wananchi wa Tanzania.
“Miradi tayari imekamilika na tunawakaribisha wananchi wote wa Dodoma na Tanzania kwa ujumla kuja kuchukua fomu kwa ajili ya uwekezaji kwa kupanga fremu za maduka na vizimba kwa ajili ya kufanya biashara” alisema Mkurugenzi Kunambi mbele ya Wanahabari.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, miradi hii imejengwa kwa takribani shilingi bilioni 89, fedha zilizotolewa na Serikali Kuu inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Mkurugenzi Kunambi amesema fomu za maombi ya maeneo ya biashara katika katika miradi hiyo zitaanza kutolewa Jumanne ya Aprili 7, 2020 katika Ofisi za Halmashauri ya Jiji za zamani.
Aidha, Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma alizungumzia suala la kuanzishwa kwa Kampuni ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma ambayo ndiyo itakayosimamia uendeshaji wa miradi huku Halmashauri ikiendelea na majukumu yake ya msingi ya kutoa huduma za kijamii kwa wakazi wa Jiji hilo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.