Picha kwa hisani ya Mtandao
HATIMAYE Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma imetekeleza azimio la Mamlaka na wadau wa Usafirishaji katika ngazi ya Wilaya na Mkoa la kuhamishia Stendi Kuu ya mabasi katika eneo la Nanenane Kata ya Nzuguni Barabara Kuu ya Dodoma-Dar es Salaam, ambapo kuanzia leo Machi 29, 2018 huduma za mabasi hayo zimeanza kutolewa katika eneo hilo.
Uamuzi huo umefikiwa kufuata eneo lililokuwa likitumika kwa muda mrefu kama Stendi Kuu kuchukuliwa na Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli Nchini (RAHCO), kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kuimarisha miundombinu ya usafiri wa Reli.
Kufuatia hali hiyo, wadau mbalimbali wa usafirishaji wakiwemo Jeshi la Polisi, Wafanyabiashara ya Usafirishaji, Mamlaka inayosimamia usafiri wa nchi kavu na majini (SUMATRA), Serikali ya Mkoa na Wilaya, pamoja na Manispaa walijadili suala hilo kwa nyakati tofauti na kukubaliana eneo la Nanenane litakidhi mahitaji ya huduma hiyo kwa sasa.
Awali, Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi aliteua ‘timu’ ya kushughulikia suala hilo na kumshauri eneo litakakidhi kutoa huduma ya usafiri wa Mikoani kwa Wananchi ili lipendekezwe, kwa kuzingatia pamoja na mambo mengine, uwepo wa miundombinu ya msingi kama Maji na Vyoo, ambapo eneo la Nanenane lilipendekezwa kwani lilishawahi kutumika kama stendi katika miaka ya nyuma.
Kaimu Mkuu wa Idara ya Ujenzi wa Manispaa ya Dodoma Mhandisi Ludigija Ndatwa amesema kuanzia leo mabasi yote ya Mikoani ni lazima yapakie na kushusha abiria wao katika stendi hiyo teule na kwamba wadau wote wameahidi kutoa ushirikiano.
“Hivi tunavyoongea nipo hapa Nanenane na wadau wote wapo hapa…wanatoa ushirikiano wa hali juu kwa kweli na kila kitu kinaenda sawa… mpaka muda huu mabasi yote yako huku kwa ajili ya kufanya safari zao” alisema Mhandisi Ludigija.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.