Na. Theresia Francis na Dennis Gondwe, DODOMA
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imeendelea kupokea wageni kutoka halmashauri nyingine wanafika kujifunza juu ya kuanzisha vyanzo vipya vya mapato ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan.
Akiongea wakati wa kuwakaribisha wageni kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Naibu Meya wa Jiji hilo, Emmanuel Chibago alisema kuwa Dodoma ilianzisha miradi mbalimbali kwa ajili ya kuongeza wigo wake wa kukusanya mapato.
Chibago alisema “nimefurahi kupata ugeni wa madiwani kutoka Manispaa ya Sumbawanga, tunashukuru kwa ujio wenu mjisikie mpo nyumbani. Ujio wenu unafungua ukurasa mpya wa uhusiano wa kiutendaji baina yetu” alisema Chibago.
Kiongozi wa msafara huo ambae ni Mstahiki Meya wa Manispaa ya Sumbawanga, Justine Malisawa alisema kuwa ziara hiyo itawajengea uwezo madiwani katika kufanya maamuzi kwenye utekelezaji wa miradi ya kimkakati. Alisema kuwa uwezo huo utakuwa katika maeneo ya kutambua gharama za miradi, utekelezaji wa miradi hiyo na kubuni vyanzo vipya vya mapato. Eneo lingine alilitaja kuwa ni usimamiaji wa mapato yanayopatikana kupitia miradi hiyo.
Aidha, aliwapongeza viongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa utekelezaji mzuri wa miradi ya kimkakati. “Ndugu zangu viongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma mmefanya kazi kubwa katika kutekeleza maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan. Tumeona na tumejifunza mambo mbalimbali kupitia miradi inayoendelea kutekelezwa jijini Dodoma. Miradi hiyo na utekelezaji wake umetupa nguvu na moyo kuona hakuna kinachoshindikana. Hata sisi tunaweza kuwekeza vyanzo vipya vya mapato katika halmashauri yetu. Tutoe wito kwa halmashauri zingine zije kutembelea Jiji la Dodoma na kujifunza” alisema Malisawa.
Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga walifanya ziara ya mafunzo katika Jiji la Dodoma kutembelea na kujifunza miradi mbalimbali inayotekelezwa katika jiji hilo kwa lengo la kuongeza wigo wa ukusanyaji mapato ikiwa ni utekelezaji agizo la Serikali kuzitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa kubuni vyanzo vipya vya mapato.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.