WASHIRIKI kutoka taasisi za Serikali, viongozi, wabunge, Asasi za Kiraia na wanafunzi wa vyuo vikuu wameshuhudia uzinduzi wa Ripoti tatu za Uwajibikaji ambazo zimetokana na Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG). Uzinduzi huo ulikuwa mubashala na kushuhudiwa pia na watu mbalimbali duniani kupitia matangazo ya mtandaoni.
Ripoti hizo zimeandaliwa na Taasisi ya WAJIBU ambayo imeziandaa ripoti hizo za uwajibikaji baada ya kuichambua kwa kina ripoti ya CAG ambayo iliwasilishwa kwa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan Machi 28 mwaka huu na baadae ripoti hiyo kukabidhiwa kwa Bunge Aprili 4 mwaka huu.
Akizungumza leo Juni 28,2021 jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya WAJIBU, Bwana Ludovic Utouh ambaye amewahi kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), amesema ripoti hizo ni za tano tangu waanze kuandaa na kuzitayarisha kutokana na ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
Utouh amezitaka ripoti hizo kuwa ni Ripoti ya Uwajibikaji Mamlaka ya Serikali za Mitaa na Miradi ya Maendeleo 2019-2020, Ripoti ya Uwajibikaji Serikali Kuu na Mashirika ya Umma 2019-2020 na Ripoti ya uwajibikaji Ufanisi, Rushwa na Ubadhilifu katika sekta ya Umma 2019-2020.
"Kama tunavyojua ripoti za mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali ambazo zimewasilishwa kwa Rais Machi 28 na kuwasilishwa Bungeni Aprili 4, ni ripoti zinazotayarishwa kitaalamu, ni kubwa na ambazo kusema kweli kwa Watanzania wangi huwa hawana shauku ya kuzisoma kwa sababu ya ukubwa wake.
Sasa sisi WAJIBU tunachukua ripoti zile na kuchambua kwa undani na tunachukua yale tunayoamini yanauzito na umuhimu mkubwa kwa watanzania, kwa hiyo utakuta ripoti ya WAJIBU iliyozinduliwa leo ya Serikali kuu na mashirika ya umma inatokana na ripoti mbili kubwa za CAG za Serikali Kuu na mashirika ya umma na tumeweza kuja na kitabu cha kurasa 31.
Na utakuta katika ripoti ile kubwa tumechambua mambo 10 ambayo tumeona yana umuhimu zaidi kwa maendeleo ya nchi yetu na ukienda kwenye ripoti ya Serikali za Mitaa na miradi ya maendeleo ambayo nayo imetokana na ripoti mbili za CAG tumetengeneza kitabu chenye kurasa 21 tu, ina mambo nane ambayo tumeona yana umuhimu kwa umma.
Ukija kwenye ripoti ya tatu ambayo ni ripoti ya Ufanisi ile kwa kuwa imetokana na ripoti ya CAG mwaka jana aliwasilisha bungeni ripoti 15 za ufanisi, sisi katika kupitia ripoti zile tumeona zina mambo muhimu zaidi kwa maendeleo ya nchi na tumeweza kuja na ripoti yenye kurasa 31 ambayo inajikita kwenye maeneo hayo," amefafanua kwa ufanisi mkubwa Utouh.
Utouh amesema ombi lake baada ya kuzinduliwa kwa ripoti hizo ni vema wananchi wakazisoma kwani wamezirahisisha na kuzipunguza ili kufanya urahisi wa kuzisoma na watazisambaza katika maeneo mbalimbali na zitakuwepo kwenye tovuti ya WAJIBU, pia zitapatikana kwenye taasisi.
"Tutazigawa kupitia taasisi mbalimbali ili watanzania wapate ripoti hizi na wazisome, wakati tunasherehekea siku 100 za uongozi wa Rais Samia kweli sisi kama wananchi wa Tanzania tuwe na ari ya kuungana naye na kumsaidia kwa nia yake njema aliyonayo ya kuleta maendeleo ya nchi katika kudai uwajibikaji,
Pale ambapo tunaona taasisi ya serikali au chombo cha Serikali hakitimizi wajibu wake, ndio lengo la WAJIBU tunasema kwamba rasimali za Serikali na taifa zikisimamiwa vizuri zinakuwa za kila Mtanzania.” Amefafanua Utouh.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Ofisi ya Msajili wa NGO's Charles Mpaka amewapongeza WAJIBU kwa kuja na ubunifu kupitia ripoti ya CAG na kuziandikia taarifa fupi. "Tumeona ripoti ya CAG ni kubwa na WAJIBU wameona umuhimu wa kuichambua na kuja na taarifa fupi. Ripoti ya CAG ilikuwa na zaidi ya kurasa 250 lakini wao wamekuja na taarifa yenye 21 mpaka 31.
Maana yake tunaongea kati ya asilimia 8 mpaka 11 zimepunguzwa, hivyo itasaidia wananchi kupata tafsiri ya haraka na uelewa mwepesi wa ripoti ya CAG," amesema Mpaka.
Bofya hapa kuzisomba ripoti hizo:
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.