Na. Faraja Mbise, DODOMA
TAASISI zilizopo Halmashauri ya Jiji la Dodoma pamoja na wananchi, wamehimizwa kupanda miti katika maeneo wanayofanyia kazi na wanayoishi ili kuifanya Dodoma iwe ya kijani na kukabiliana na madiliko ya tabia ya nchi.
Hayo yalisemwa na Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Kaspar Mmuya alipokuwa akizungumza na wadau mbalimbali katika zoezi la upandaji miti kwa awamu ya pili lililohusu wazaliwa wa mwezi Novemba lililofanyika tarehe 18 Novemba, 2024 katika eneo la Jakaya Kikwete Square, Chuo Kikuu cha Dodoma.
“Tumeshaanza kuyagundua maeneo kama matatu hivi, lakini hili ni la pili tutatekeleza Januari au Februari, tayari tumeshaongea na Halmashauri ya Jiji la Dodoma na watatupatia. Maeneo katika Jiji la Dodoma yapo, Dodoma kuwa kijani inawezekana. Watu wanaishi na historia kuwa Dodoma haistawi, ni kavu, ni kame. Hapana, Dodoma sio kame na mifano ipo, mimi ninawaambieni, tafuteni muda, mzunguke mitaani muangalie kwenye nyumba za watu, zilizowekewa fensi utakuta ndani kuna miti kijani kabisa, lakini nje ya fensi hakuna miti ya kijani. Nawapongeza watu wote wanaofanya hivi kwasababu ilikuwa ni agizo la Jiji la Dodoma, kuna sheria ndogo iliyoundwa katika kila kibali cha ujenzi unachopewa ni lazima upande miti isiyopungua mitano ikiwemo miti ya matunda na miti mingine ya vivuli”
Aidha, aliwashukuru wadau mbalimbali kwa kuunga mkono kampeni ya ‘Mti wangu, Birthday yangu’ kwa kusaidia kutoa miti na maji kwa ajili ya kuunga mkono jitihada hiyo ya kuifanya Dodoma kuwa ya kijani na kukabiliana na madiliko ya tabia ya nchi. “Naomba nichukue fursa hii bila kupepesa macho, niwashukuru sana NMB, walipewa jukumu na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, kuwa miti hii waendelee kuitunza, lakini Chuo Kikuu cha Dodoma ndio wenye eneo hili, nao kila siku wapo hapa wakisaidiana na timu ya wataalamu wa UDOM na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa. Ninawashukuru sana kwa malezi mazuri ambayo miti hii mmeipa, ninawashukuru sana watu wa (TANESCO) hii ni mara ya pili mnakuja kwa wingi, nawapongeza sana (TARURA) na taasisi zingine zote zilizofika, naombeni katika ofisi zenu pia mkapande miti. Sio muda wote tunakuwa kazini wakati mwingine tunapumzika kwahiyo pangeni siku mpande miti na Taasisi zote zillizopo Dodoma tuhakikishe kwenye ofisi zetu zote tupande miti” alisisitiza Mmuya.
Akiongelea kuhusu maendeleo ya upandaji miti katika eneo lililotengwa, kuanzia Oktoba mpaka sasa Novemba, Mhandisi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, David Chitemo, alitoa tathimini kwa ujumla ya zoezi zima.
“Tumezindua zoezi hili la “Mti wangu, Birthday yangu” mwezi wa kumi, ambayo ilikuwa siku ya kuzaliwa Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, tulianza wa kusafisha eneo ambalo lina ukubwa wa ekari saba, eneo lote lina ekari kumi, na bado kuna ekari tatu zinazoendelea kusafishwa. Awamu ya kwanza katika uzinduzi tulipanda mita 780, iliyiohusisha miti ya matunda na miti mingine ya vivuli, tulipopata wadau wengine tuliongeza haya mashimo 492 ambayo ndio tumepanda leo. Hiyo, miti tuliyopanda mwezi wa kumi ni miti saba tu ndio iliyokufa, miti maji miwili, miembe miwili, mijohoro miwili na mzambarau mmoja. Lakini yote tulisha ‘replace’ kuweka mipya. Changamoto ni maji, tunawashukuru wote kila mmoja kwa jitihada zake na kwapamoja tutashinda. Leo tumepanda miti 492, kwasasa hakuna shimo lililobaki bila mti” alisema Chitemo.
Kwa upande wake Afisa Msaidizi uduma kwa wateja (TANESCO) Dodoma, Regina Mkalawa alitoa rai kwa watanzania kutunza mazingira kwa kubainisha faida za utunzaji miti na kutotumia nishati chafu ya kupikia kama kuni na mkaa ikiwa ni juhudi ya kuunga mkono kampeni ya matumzi ya nishati safi ya kupikia, iliyoanzishwa na Rais wa Jamhuri ya Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Sisi kama wadau, TANESCO Mkoa wa Dodoma, tumehamasika kwa kiasi kikubwa sana kwasababu tunajua umuhimu wa upandaji miti na tunajua faida za miti. Miti ni kichocheo kikubwa cha mvua, tunapokuwa tunaharibu miti yetu au misitu tunachangia kwa asilimia kubwa kutopata mvua ya kutosha. Na tunapokuwa tunapanda miti kwa wingi tunajiwekea asilimia kubwa ya mvua kunyesha.
Akizungumzia suala la nishati safi ya kupikia, aliwataka wananchi kutunza mazingira na kuacha kukata miti ovyo kwa ajili ya kuni na mkaa ambayo hupelekea changamoto ya kiafya hasa kwa akina mama wanaotumia nishati chafu ya kupikia. “Umuhimu mkubwa wa kutumia nishati safi ya kupikia kwanza inaturahisishia kazi za jikoni, mwanamke anaetumia jiko la mkaa yaani nishati chafu na anaetumia nishati safi ya kupikia tofauti yao katika muda ni kwamba mwanamke anaetumia nishati safi badala ya kutumia dakika 30 kupika chakula atatumia labda dakika 15 lakini anaetumia mkaa atatumia karibu lisaa lizima. Kwahiyo, nishati safi imesaidia kurahisisha muda ambao unaupoteza na utafanya majukumu mengine ya kimaendeleo. Changamoto ya kutumia nishati chafu ya kupikia inapunguza umri wa kuishi, mama atapuliza mkaa kwa muda mrefu atapata kifua, atapata magonjwa pia ‘life span’ inapungua, labda tunasema ‘life span’ ya mtanzania kwa sasa ni miaka 45, sasa baada ya mama kuishi miaka hiyo ataishi labda miaka 30 na yote hii ni kwasababu ya matumizi ya nishati chafu ya kupikia” alisisitiza Mkalawa.
Vilevile, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma ambae pia ni mdau wa Mazingira na Katibu wa Klabu ya Mazingira Endelevu (ESCUDOM), Agape Latyandumi aliwataka wananchi kutunza na kuthamini Mazingira kwa kupanda miti ili kuepukana na majanga ya asili kutokana na hali ilivyo kwasasa ya mabadiliko ya tabia ya nchi.
“Niko hapa kuwaambia wananchi na watanzania kwa ujumla tupende kutunza Mazingira na ‘kusupport’ kampeni hii ya kupanda miti ili kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa yaliyojitokeza kwa sasa. Natoa wito kwa wananchi kuwa kila mtu aliye na mti nyumbani autunze na kama hana mti inahitajika apande mti katika eneo analoishi ili kuunga mkono kampeni hii ya upandaji miti katika Mkoa wetu wa Dodoma” alisema Latyandumi.
Kampeni hii ya ‘Mti wangu, Birthday yangu’ ilizinduliwa rasmi Oktoba 18, 2024 na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, kwenye eneo la Jakaya Kikwete Square ndani ya Chuo Kikuu cha Dodoma, yenye lengo la kuifanya Dodoma iwe ya kijani ambapo imewakutanisha wadau mbalimbali wa Mazingira, wanafunzi pamoja na wazaliwa wa mwezi Novemba. Miti 780 ilipandwa kwenye eneo la ekari saba wakati wa uzinduzi wa kampeni na mwezi Novemba jumla ya miti 492 imepandwa.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.