Taasisi zote za Serikali na binafsi zimesisitizwa kuwepo kwa usawa wa kijinsia mahala pa kazi hususan katika shughuli zote za maendeleo ikiwemo nafasi za maamuzi, siasa na umiliki wa mali ikiwemo ardhi.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo kimkoa yamefanyika wilaya ya Kondoa.
Aidha, Senyamule amesema mkoa wa Dodoma unajumla ya idadi ya watu 3,083,625 ambapo wanawake ni asilimia 51 na wanaume asilimia 49 ambapo mikakati ya Serikali ni kuona ifikapo 2030 nafasi ya mwanamke iwe imefikia asilimia 50 kwa 50 katika masuala mbalimbali yakiwemo masuala ya maamuzi na maendeleo ya kiuchumi.
Senyamule amesema lengo la kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani ni kutaka kuhamasisha jamii juu ya uwezo wa wanawake katika kuleta Usawa wa Kijinsia na maendeleo ya kiuchumi.
Katika hatua nyingine, Senyamule amesema wanawake ni Jeshi kubwa wakiwezeshwa wanaweza na wamesisitizwa kuepuka vishawishi vya kuingia kwenye ndoa za jinsia moja.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Maadhimisho ya Mkoa wa Dodoma, Penina Robert amesema amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kwa kuwawezesha wanawake kupata mikopo ya riba nafuu na amewaomba wanawake kote nchini kuungana kwenye vikundi ili kuepuka mikopo umiza.
Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani huadhimishwa kila mwaka tarehe 8, Machi, mwaka huu 2023 yamebebwa na Kaulimbiu isemayo "Ubunifu na Mabadiliko ya Teknolojia Chachu katika kuleta Usawa wa Kijinsia" ambapo zaidi ya Taasisi 97 kutoka mkoa wa Dodoma zimeshiriki.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.