WASHIRIKI katika kukimbiza Mwenge maalum wa Uhuru mwaka 2021 wametakiwa kuvaa barakoa na kuchukua tahadhari zote dhidi ya ugonjwa wa UVIKO-19.
Ushauri huo ulitolewa na Kiongozi wa mbio za Mwenge Maalum wa Uhuru mwaka 2021, Lt. Josephine Mwambashi alipoongoza timu yake ya wakimbiza Mwenge maalum wa Uhuru kitaifa kuingia Wilaya ya Dodoma katika eneo la Makutopora leo.
Lt. Mwambashi alisema kuwa ugonjwa wa UVIKO-19 upo. “Katika kukabiliana na tahadhari ya ugonjwa huo ni muhimu kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono. Na wote tunaokimbiza Mwenge maalum wa Uhuru tuwe tumevaa barakoa” alisema Lt. Mwambashi.
Kila msoma taarifa ya mradi, baada ya kuisoma atabaki na taarifa hiyo, hataikabidhi kwa Kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa, aliongeza. “Kwenye miradi hasa ya majengo tutaingia watu wachache ili kujipa nafasi” alisema Lt. Mwambashi.
Akikiri kuupokea Mwenge maalum wa Uhuru mwaka 2021, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri alisema “nakiri kuupokea Mwenge maalum wa Uhuru kutoka kwa Mheshimiwa Dkt. Khamis Mkanachi, Mkuu wa Wilaya ya Kondoa ukiwa unawaka na kumeremeta”. Alisema kuwa ukiwa wilayani Dodoma, Mwenge huo utakimbizwa umbali wa kilometa 101 na utapitia miradi mitano ya maendeleo yenye thamani ya shilingi 28,491,637,324.
Wakati huohuo, Shekimweri aliwapongeza wakimbiza Mwenge hao kwa kuaminiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kukimbiza Mwenge maalum wa Uhuru kitaifa mwaka 2021.
Mwenge Maalum wa Uhuru mwaka 2021 unaongozwa na kaulimbiu isemayo “TEHAMA ni msingi wa Taifa endelevu; itumie kwa usahihi na uwajibikaji”. Mapokezi ya Mwenge huo yaliongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, na kushuhudiwa na Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, viongozi wa CCM Wilaya, Wabunge, Kamati ya Usalama ya Wilaya, Mkurugenzi wa Jiji, Madiwani, Timu ya Wataalam ya Halmashauri, Watumishi wa Jiji la Dodma na mamia ya wananchi wa Wilaya ya Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.